Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewataka wananchi nchini kuhakikisha wanamiliki ardhi zao kisheria, ikieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo amesema umiliki rasmi wa ardhi unasaidia kulinda haki za wananchi, kuongeza thamani ya maeneo yao pamoja na kuweka mazingira salama ya uwekezaji na uzalishaji.
Akizungumza leo Mei 28,2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Dkt. Akwilapo amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kurasimisha umiliki wa ardhi ili wananchi wengi zaidi waweze kupata hati na nyaraka halali za maeneo yao.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 wizara ilijiwekea lengo la kuandaa na kusajili hatimiliki 500,000, kutoa hati za hakimiliki ya kimila 520,000, hati za sehemu ya jengo 1,000 pamoja na vyeti vya ardhi ya vijiji 100 na kushughulikia miamala ya hatimiliki na nyaraka za kisheria 100,000.
Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, hadi Mei 15, 2026 wizara ilikuwa imeandaa na kusajili hatimiliki 107,683 sawa na asilimia 21.54 ya lengo, huku hati za hakimiliki ya kimila zilizotolewa zikifikia 99,762 sawa na asilimia 19.19.
Aidha, amesema wizara imefanikiwa kuvuka lengo la utoaji wa vyeti vya ardhi ya vijiji baada ya kutoa vyeti 148 sawa na asilimia 148 ya utekelezaji, jambo alilosema linaonesha mafanikio ya jitihada za serikali katika kuimarisha usimamizi wa ardhi vijijini.
Katika hatua nyingine, hati za sehemu ya jengo zilizotolewa zimefikia 914 sawa na asilimia 91.4 ya lengo, huku serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kurasimisha umiliki wa ardhi zao ili kuzitumia kama mtaji wa maendeleo na kujihakikishia usalama wa maeneo yao kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Comments
Post a Comment