MISUNGWI, MWANZA
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta za kilimo na mifugo kwa kuanzisha shughuli za uzalishaji zitakazowaongezea kipato, kuimarisha uchumi wa familia na kuwaandaa kwa maisha bora baada ya kustaafu.
Wito huo ulitolewa katika kikao cha kawaida cha watumishi kilichoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Addo Missama, mwishoni mwa wiki, wakati wa kujadili utekelezaji wa mipango ya mwaka wa fedha 2026/2027 ulioanza Julai 1, 2026.
"Watumishi tusisubiri muda wa kustaafu ndipo tuanze kufikiria chanzo kingine cha kipato. Tumejaliwa wataalamu wa kilimo na mifugo ndani ya halmashauri; watumieni kupata ushauri wa kitaalamu na anzeni kuwekeza mapema," alisema Katabazi.
Alisema hatua hiyo itawasaidia kujijengea utulivu wa kifedha na kujiandaa vyema kwa maisha ya kustaafu.
Aidha, aliwahimiza kutumia muda wanaoupata baada ya saa za kazi kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kuwataka kutumia wataalamu wa kilimo na mifugo waliopo halmashauri kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu mbinu bora za kilimo na ufugaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Addo Missama, aliwataka watumishi kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uadilifu na kuwajibika, akisisitiza kuwa hakuna haki bila kutimiza wajibu.
"Hakuna haki bila wajibu. Kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa," alisema Missama.
Alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya halmashauri hiyo, hivyo aliwataka watumishi wa idara zote kushirikiana kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Missama alisema Halmashauri ya Misungwi ilifanikiwa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na kufikia Sh bilioni 4.76 katika mwaka wa fedha 2025/2026 kutokana na ushirikiano mzuri wa watumishi na wadau mbalimbali.
"Katika mwaka mpya wa fedha, tumejipanga kuongeza zaidi mapato ya ndani, kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria na taratibu," alisema.
Naye Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Bi. Samina Gullam, aliwataka watumishi kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kutumia ipasavyo muda wa kazi, kuimarisha ushirikiano mahali pa kazi na kudumisha upendo.
"Menejimenti itaendelea kuhakikisha mazingira bora ya kazi yanaboreshwa na mahitaji muhimu ya watumishi yanashughulikiwa kwa kuzingatia bajeti na miongozo ya Serikali. Tunahitaji ushirikiano wa kila mmoja ili kufanikisha malengo ya mwaka wa fedha 2026/2027," alisema Gullam.











Comments
Post a Comment