Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amepiga marufuku tabia ya kuwatoza wagonjwa fedha za mafuta wanapohitaji kusafirishwa kwa magari ya wagonjwa (ambulance), akisema kitendo hicho kinakiuka sheria, sera na maelekezo ya Serikali.
Ametoa kauli hiyo leo Julai 4, 2026, alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Suguti, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, ambapo aliwaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha hakuna mgonjwa anayekwamishwa kupata huduma za rufaa kwa kuombwa fedha za mafuta.
"Ambulance ipo, mnamwambia mgonjwa achangie mafuta. Haya ni mambo yanayokiuka sheria, yanayokiuka sera na yanayokiuka maelekezo. Haya ni mambo yasiyokubalika," alisema Waziri Mkuu.
Alisema Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa hospitali, ununuzi wa magari ya wagonjwa, ajira za wataalamu wa afya na kuboresha upatikanaji wa dawa, hivyo hakuna sababu ya wagonjwa kucheleweshwa kupata matibabu kwa kuombwa fedha za mafuta.
"Unamuombaje mafuta mgonjwa mahututi? Unamcheleweshaje mgonjwa kwa sababu ya mafuta? Hili halikubaliki. Ikitokea mgonjwa amezidiwa, ambulance ipo halafu akacheleweshwa kwa sababu ya mafuta, tupate huyo aliyemchelewesha ili ajulikane ameshindwa kazi," alisisitiza.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma kuongeza uwajibikaji na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati, akisisitiza kuwa ziara za viongozi haziwezi kuwa mbadala wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali.
"Nimeelekeza kwamba ziara si mbadala wa kazi za Serikali. Lazima kazi za kutatua kero za wananchi ziendelee kila siku. Hatuwezi tukawa tunatatua kero kwa ziara tu," alisema.
Aidha, Waziri Mkuu alielekeza kuharakishwa kwa taratibu za kimkataba ili ujenzi wa awamu ya kwanza ya kilometa 40 za barabara ya Musoma–Suguti–Makojo–Busekera uanze kwa wakati, sambamba na kusisitiza matumizi sahihi ya fedha za umma na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi hiyo inatoa thamani halisi kwa wananchi.
Vilevile, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kulinda amani, utulivu na mali za umma, akieleza kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
"Amani na usalama wa eneo lako, mnufaika wa kwanza ni wewe mwenyewe. Tukilinda amani, tunalinda maendeleo yetu," alisema.










Comments
Post a Comment