Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, ameipongeza menejimenti ya Chuo cha Elimu ya Biashara CBE kwa uongozi mzuri na maendeleo yaliyopatikana ndani ya kipindi cha muda mfupi.
Naibu Waziri Katambi aliyasema hayo jana jijini Dar es salaam, alipotembelea chuo hicho ikiwa mwendelezo wa ziara zake za kujitambulisha kwenye taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara hiyo.
“Marais wote waliopita waliona umuhimu wa kuendeleza chuo hiki nawapongeza nyinyi kwa mpango mkubwa wa upanuzi wa chuo na katika utoaji wa huduma kwa watanzania. Mmeweza kwenda Dodoma, Mwanza, Mbeya na sasa Kilimanjaro ni hatua kubwa sana kuwafikia kokote waliko badala ya wote kulazimika kuja Dar es Salaam wanasoma huko huko waliko,” alisema.
Alisema CBE imefanikiwa kuongeza madarasa, maeneo ya wazi ya kupumzikia, kupanua maeneo ya madarasa majengo ya utawala na maeneo ya bweni.
“Nimeona jengo kubwa la metrolojia litakalogharimu shilingi bilioni 26 ambalo limefikia zaidi ya asilimia 88 ya ujenzi wake ni hatua kubwa sana nawasisitiza waliosoma CBE wawe mabalozi wazuri wa chuo hiki ili na watu wa nje ya nchi waje kusoma hapa,” alisema Katambi.
“Mmeniambia kuwa mmefanikiwa kutoa machapisho 148 ambayo kwa kweli yanaifanya CBE itambulike kimataifa, mna Shahada za Uzamivu zaidi ya 52 na wanafunzi zaidi ya 23,000 hili ni jambo la kupongeza sana kwasababu taifa lolote ili liweze kuendelea lazima liwe na wasomi wa nyanja mbalimbali,” alisema.
Naibu Waziri aliwataka wanafunzi wa chuo hicho kujiamini na kuhakikisha wanasimamia na kutimiza ndoto zao.
Aliwasisitiza kuweka mkazo kwenye masomo yao kwa kuhakikisha wanafaulu kwa kiwango cha juu ili waweze kushindana kitaifa na kimataifa zinapotokea nafasi za ajira.
Alisema serikali inaendelea kuweka mazingira mazurikwa wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini kupata ajira na wengine kujiajiri mara wanapohitimu masomo yao.
Alisema ni wajibu wa kila mwanafunzi kuhakikisha anafuatilia mambo ya msingi chuoni na kuachana na mambo yasiyo ya msingi yanayoweza kumkwamisha kuhitimu.
Alisema kinachoweza kumfanya mwanafunzi akafanya vizuri kwenye masomo yake siyo uzuri wa majengo bali bidii aliyoiweka kwenye masomo yake akisisitiza kuwa watu waliosoma zamani walisomea kwenye majenego chakavu lakini walikuwa wakifaulu kwa alama za juu.
Kadhalika, Katambi alipongeza menejimenti ya CBE kwa namna inavyosimamia rasilimali za chuo hicho na maboresho makubwa waliyofanya ndani ya muda mfupi.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga alisema chuo hicho tayari kimeanza maandalizi ya ujenzi wa kampasi ya Kilimanjaro ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 mkoani humo.
Alisema tayari chuo hicho kimeshampata mkandarasi mshauri kwaajili ya kuchora michoro ya kampasi hiyo ambapo wanatarajia kuanza na majengo ya utawala, majengo ya mafunzo na mabweni ya wanafunzi.
Alisema wanatarajia eneo hilo litakuwa kituo mahiri cha ukarimu na utalii kwa kufundisha masomo ya biashara, utalii na ukarimu na kwamba chuo hicho pia kinatarajia kupata fedha za mradi wa HEET zinazotolewa na Benki ya Dunia (WB).







