Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameipongeza Kampuni ya Soya One Limited pamoja na Eliakim Maswi kwa kujitolea kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule za sekondari wilayani humo, akisema mchango huo ni kielelezo cha uzalendo na unaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Meja Gowele amesema Serikali ya Wilaya inaamini maendeleo ya elimu hayawezi kuachwa mikononi mwa Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo wawekezaji, wafanyabiashara, viongozi wa kisiasa na wananchi.
Amesema kila mwenye uwezo anapaswa kuchangia maendeleo ya elimu kwa kiwango anachoweza, akisisitiza kuwa hakuna mchango mdogo unapolenga kuboresha maisha ya watoto na mustakabali wa Taifa.
"Sio lazima uwe na uwezo mkubwa ndiyo uchangie elimu. Hata mchango mdogo unaweza kuleta mabadiliko makubwa. Tunawapongeza Soya One Limited na Eliakim Maswi kwa moyo wao wa kujitolea. Huu ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na wadau wengine," amesema Meja Gowele.
Amesema vifaa hivyo vitasaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hususan katika uchapishaji wa mitihani na matumizi ya teknolojia shuleni, hivyo kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili walimu.
Aidha, amewahimiza walimu kuvitunza na kuvitumia kwa ufanisi ili viweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa, huku akiwataka wazazi na viongozi wa ngazi zote kuendelea kushiriki katika maendeleo ya elimu.
"Madini yanaweza kuisha, lakini elimu haiishi. Tukiwekeza kwenye elimu leo, tunajenga kizazi kitakacholiletea Taifa maendeleo ya kudumu," amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Soya One Limited, Chacha Soya, amesema kampuni hiyo imeamua kushiriki katika maendeleo ya elimu kwa kutambua kuwa uwekezaji kwa watoto ni uwekezaji kwa mustakabali wa Taifa.
Alieleza kuwa utoaji wa vifaa hivyo umetokana na ushirikiano kati ya kampuni yake na Eliakim Maswi, ambaye alimpongeza kwa moyo wake wa kujitolea kurudisha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii.
"Tunafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha tunatafuta fursa za kusaidia jamii. Elimu ni msingi wa maendeleo, hivyo tutaendelea kushirikiana na Serikali pale tutakapohitajika," amesema Chacha Soya.
Amesema mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamewapa hamasa wawekezaji kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii, akiwataka viongozi kuendelea kuwakaribisha na kuwapa ushirikiano wawekezaji wanaotaka kuisaidia jamii.
Chacha Soya pia amewataka viongozi wa kisiasa kuweka tofauti zao pembeni na kushirikiana katika kuendeleza elimu, akisema maendeleo ya watoto hayapaswi kuathiriwa na tofauti za kiitikadi.
"Tunapofanya jambo jema kwa jamii tunahitaji ushirikiano na faraja kutoka kwa viongozi na wananchi. Tukishirikiana, tutafanya mengi zaidi kwa ajili ya watoto wetu na Taifa kwa ujumla," amesema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Juster Magabe, aliwashukuru Soya One Limited na Eliakim Maswi kwa moyo wao wa uzalendo, akisema msaada huo utachochea maendeleo ya elimu na kuongeza ari ya wanafunzi na walimu.
Amesema Halmashauri itahakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kusimamiwa ipasavyo ili viweze kuwanufaisha wanafunzi wengi zaidi.
"Kwa niaba ya madiwani na wananchi wa Tarime, tunawashukuru sana Soya One Limited na Eliakim Maswi kwa moyo wao wa kujitolea. Tunaahidi kusimamia matumizi sahihi ya vifaa hivi ili viwe na manufaa ya kudumu kwa shule zetu," amesema Magabe.
Ameongeza kuwa mchango huo unaonesha namna ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii unavyoweza kuharakisha maendeleo ya elimu, huku akitoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo kwa kuendelea kuwekeza katika elimu ya watoto wa Tarime na Tanzania kwa ujumla.
Vifaa vya TEHAMA vilivyotolewa vinatarajiwa kuboresha utoaji wa huduma za elimu katika shule mbalimbali za sekondari wilayani Tarime, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na kujifunzia sambamba na kuunga mkono dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuinua ubora wa elimu nchini.





Comments
Post a Comment