Zungu atoa saluti kwa vyombo vya ulinzi nchini, aipongeza bajeti ya trilioni 4.28 kwa Wizara ya Ulinzi na Jkt
Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yenye thamani ya Shilingi Trilioni 4.28 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, akiipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha sekta ya ulinzi na usalama nchini.
Akizungumza Mei 19, 2026 bungeni Jijini Dodoma mara baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Zungu alisema ameridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Ulinzi pamoja na vyombo vya ulinzi katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani, utulivu na usalama.
Spika huyo alimpongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho, kwa uongozi wake madhubuti na usimamizi mzuri wa wizara hiyo nyeti, akieleza kuwa utekelezaji wa majukumu ya wizara umeendelea kuleta mafanikio makubwa kwa taifa.
“Tunajivunia kazi kubwa inayofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi katika kulinda mipaka ya nchi, kudumisha amani na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama muda wote,” alisema Zungu.
Aidha, amewapongeza pia viongozi na maafisa wa vyombo vya ulinzi wakiongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jacob Mkunda, kwa kujitolea kwao katika kuimarisha usalama wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.


Comments
Post a Comment