Waziri Mavunde Asimamisha Uchimbaji wa Madini kwenye Mto Katavi

GEORGE MARATO TV
0



▪️Ni kutokana na mapungufu ya mpango wa usimamizi wa mazingira

▪️Aelekeza kupewa hati za makosa wamiliki wa Leseni za Utafiti mkoani Katavi

▪️Aelekeza ukaguzi wa mikataba ya msaada wa kiufundi(TSA) nchi nzima

▪️Wachimbaji wadogo wampongeza Rais Samia kwa kupatiwa Leseni tatu kubwa zilizofutwa

▪️Ziara hii ya utatuzi wa migogoro ni maelekezo ya Waziri Mkuu Mwigulu aliyotoa mkoani Katavi

▪️Wachimbaji waishukuru serikali kwa utatuzi wa changamoto zilizokuwa zinawakabili


*Katavi*

Kufuatia ukaguzi uliofanywa kwa wamiliki wa leseni wanaofanya uchimbaji kwenye mto na kuathiri mazingira, Waziri wa Madini *Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)* atoa maelekezo ya kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji madini kwenye mto huo Mkoani Katavi.

Ametoa kauli hiyo tarehe 13 Mei, 2026 alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za uchimbaji madini katika Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Nsimbo Mkoani Katavi.



"Mhe. Rais ametupa maelekezo mahsusi Wizara ya Madini kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika kwa mujibu wa Sheria na zisilete athari kwenye mazingira. Tumeshuhudia sote kinachofanyika hapa ni kinyume na matakwa ya Sheria yetu ya Madini Sura 123"

"Hivyo, naelekeza kuanzia leo shughuli zote za uchimbaji zisimame mpaka pale mtakapotekeleza wajibu wenu kama mlivyoelekezwa na Afisa Madini Mkazi wa Katavi kupitia barua aliyowaandikia. Pia, wamiliki wa leseni wasilisheni mpango wa kuhifadhi mazingira kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji tena", alisisitiza Waziri Mavunde.



Vilevile, Waziri Mavunde alifanya ukaguzi wa mikataba ya msaada wa kiufundi (TSA) waliyoingia wachimbaji wadogo wa kitanzania na wawekezaji wa nje na kubaini mapungufu ambayo yalipelekea kuagiza Ofisi za Afisa Madini Wakazi wa Mikoa ya kimadini kufanya ukaguzi wa mikataba ya TSA nchi nzima ili kubaini iwapo inawanufaisha watanzania na inazingatia matakwa yaliyowekwa kisheria.

Akieleza utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa maeneo ya uchimbaji, *Mhe. Mavunde* alitoa maelekezo kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kutoa Hati ya Makosa (Default Notice) kwa wamiliki wote wa leseni za utafiti wasioendeleza na kufuata masharti ya leseni hizo.

"Lengo ni kuyafuta maeneo yote ya leseni za utafiti yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo kupitia vikundi vyao. Aidha, maeneo mengine yatatumika kugawa maeneo kwa wachimbaji wadogo vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia programu ya Mining for A Brighter Tommorow (MBT)" alibainisha Waziri Mavunde.





Akibainisha juu ya leseni alizozifuta mwezi uliopita, Waziri Mavunde alitangaza kutenga leseni 3 za utafiti ili zigawiwe kwa wachimbaji wadogo Mkoani Katavi, ambapo wachimbaji wadogo walishukuru na kupongeza jitihada zinazofanywa na *Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan* za kuwasikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa wakati.

Awali, Mhe. Mavunde alieleza kuwa amefika kufanya ziara Mkoani Katavi kufuatia maelekezo ya *Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb)*, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa alipofanya ziara ya kikazi Mkoani Katavi.

Akitoa maelezo ya Mkoa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, *Mheshimiwa Onesmo Buswelu* aliishukuru Serikali kwa hatua za utatuzi wa changamoto za wachimbaji Mkoani Katavi na kuahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Madini yanakwenda kusimamiwa ipasavyo ili yalete tija na kuimarisha shughuli za uchimbaji.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, *Mheshimiwa Haidary Sumry* na *Mheshimiwa Anna Lupembe*, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo walimshukuru *Mhe. Rais* kwa kuendelea kuisimamia ipasavyo Serikali ambayo imekuwa ni mhimili imara katika kutatua changamoto za wananchi wa majimbo yao.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top