WAZEE na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wameendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda amani ya nchi, wakionesha kuunga mkono Tume ya Rais , wakisema ni hatua muhimu inayotokana na mahitaji ya wananchi wenyewe na si Serikali pekee au Rais Samia Suluhu Hassan.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamesema kuwepo kwa dalili za mgawanyiko wa kijamii kunahitaji juhudi za makusudi za kurejesha mshikamano, kupitia majukwaa ya kusikilizana, kujenga imani upya na kuimarisha umoja wa taifa.
Dkt. Daniel Ouma, mkazi wa Mkoa wa Mara, amesema ni wakati wa Watanzania kuweka tofauti zao pembeni na kuangalia maslahi ya taifa kwa ujumla.
“Ni wakati wa Watanzania kuweka tofauti zao pembeni na kujenga maridhiano kwa ajili ya mustakabali wa nchi,” amesema.
Mzee Festo Paulo amesema amani ni msingi wa maendeleo ya kweli, akisisitiza kuwa kila Mtanzania ana jukumu la kuilinda.
“Nchi isiyo na amani haina maendeleo. Ni wajibu wa viongozi na wananchi kwa pamoja kuhakikisha tunaidumisha amani na kufuata njia sahihi za maisha,” amesema.
Kwa upande wao, Juma Masiroli na Mzee Festo Paulo wamesema utulivu na ushirikiano vinapaswa kuendelea kuwa nguzo ya jamii katika kushughulikia changamoto za kitaifa.
“Tumeonesha utulivu siku zilizopita, ni vyema tuendelee hivyo ili kutoa nafasi kwa serikali kushughulikia changamoto zilizopo,” wamesema.
Aidha, wameonya dhidi ya tabia ya kupinga kila jambo, wakieleza kuwa hali hiyo inaweza kudhoofisha mshikamano wa kitaifa.
“Huu si wakati wa kuonesha ishara za kukataa kila kitu, bali ni wakati wa kujenga pamoja na kushirikiana kwa busara,” wameongeza.
kauli za wazee hao zimebeba ujumbe wa umoja, uvumilivu na mshikamano, zikisisitiza kuwa amani ni msingi mkuu wa maendeleo ya Taifa.



