NAIBU Waziri wa Elimu na Teknolojia ya Habari, Wanu Hafidh Ameir, amekutana na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Chemuchemu jijini Dodoma waliotembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujifunza namna chombo hicho kinavyofanya kazi.
Katika ziara hiyo ya kielimu, wanafunzi walipata fursa ya kusikiliza maelezo kuhusu shughuli za Bunge, huku wakihamasishwa kujituma katika masomo yao ili kuwa viongozi bora wa baadaye.
Baada ya mazungumzo hayo, Naibu Waziri alipiga picha ya pamoja na wanafunzi hao kuadhimisha kumbukumbu ya ziara yao.
Awali, Afisa Mwandamizi wa Elimu kwa Umma wa Bunge, Waziri Kizingiti, alitoa maelekezo kwa wageni hao kuhusu taratibu za Bunge na namna ya kufuatilia vikao kwa utulivu na nidhamu.
Wakiwa ndani ya Ukumbi wa Msekwa, wanafunzi hao walipata elimu ya kina kuhusu mwenendo wa Bunge, sambamba na fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ili kuongeza uelewa wao.
Aidha, walihudhuria kipindi cha maswali na majibu ndani ya ukumbi mkubwa wa Bunge, wakishuhudia moja kwa moja namna wabunge wanavyowasilisha hoja na kujibiwa na Serikali.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala ya utawala na demokrasia, huku ikiwapa hamasa ya kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.









Comments
Post a Comment