Uchaguzi mdogo EALA kufanyika Mei 5,2016

GEORGE MARATO TV
0


 
KATIBU wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraka Leonard, ametangaza rasmi kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kuchagua wajumbe watatu watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), utakaofanyika Mei 4, 2026.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo April 30,2026 katika Ofisi za Bungeni Jijini Dodoma, katibu wa Bunge Baraka Leonard
Amesema uchaguzi huo unalenga kujaza nafasi zilizoachwa wazi kufuatia James Kinyasi Millya, Dkt. Ng’waru Jumanne Maghembe, na Angela Charles Kizigha kuwa wabunge wa Bunge la Tanzania.


“Kwa mujibu wa sheria, wabunge hawa wamekoma kuwa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki mara baada ya kuapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Tanzania,” amesema.

Ameeleza kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa kuzingatia kanuni na sheria mbalimbali za Bunge pamoja na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku ukilenga kuhakikisha nafasi zilizo wazi zinajazwa kwa wakati na kwa kuzingatia uwakilishi wa makundi maalum.

“Uchaguzi huu unafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa kisheria, na unazingatia uwakilishi wa makundi kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za Bunge na Mkataba wa Jumuiya,” amesisitiza.

Amefafanua kuwa nafasi zinazogombewa zinahusisha kundi la wanawake lenye nafasi moja pamoja na kundi la Tanzania Bara lenye nafasi mbili, ambapo wagombea waliokidhi vigezo na kupitishwa ni Fatuma Abdallah Kange, anayewania nafasi ya wanawake, na Cosato David Chumi pamoja na Kambarage Masato Wasira, wanaowania nafasi za Tanzania Bara.

“Baada ya kupitia sifa na vigezo vinavyotakiwa kisheria, nimeridhika kuwa wagombea hawa wanastahili kushiriki katika uchaguzi huu,” amesema.


Ameongeza kuwa siku ya uchaguzi wagombea wataruhusiwa kujitambulisha mbele ya wabunge na kuomba kura kwa lugha ya Kiingereza, kabla ya wabunge kupewa nafasi ya kuwauliza maswali ya papo kwa papo, na hatimaye zoezi la upigaji kura kuanza.

“Baada ya hatua hizo, kura zitapigwa, kuhesabiwa na washindi watatangazwa rasmi,” ameeleza.

Aidha, ametoa wito kwa vyombo vya habari kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu mchakato huo ili kuongeza uelewa na ushiriki wa umma.

“Ni muhimu wananchi wakafahamu namna wawakilishi wao wanavyopatikana ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuwajibisha viongozi wao,” amesema.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top