Tiba asili yapata Heshima Mpya serikalini,Dkt.Eyembe Aipongeza Serikali

GEORGE MARATO TV
0

 

MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora (Kitete), Dkt. Joackim Eyembe, amepongeza hatua ya Serikali kuendelea kuitambua na kuipa nguvu huduma ya tiba asili na tiba mbadala kupitia Bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka wa fedha 2026/2027, akisema hatua hiyo ni mwanzo wa mapinduzi makubwa katika sekta ya afya nchini.

Akizungumza katika Viwanja vya Bunge  kufuatia hotuba ya Bajeti iliyowasilishwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa Mei 11, 2026, Dkt. Lyembe amesema tiba asili imekuwa msaada mkubwa kwa jamii tangu zamani kabla ya uwepo wa hospitali kubwa za kisasa.

“Tulikuwa tunaamini tiba nyingi zinapatikana hospitalini pekee, lakini ukweli ni kwamba hata kabla ya kuwepo kwa hospitali hizi kubwa za rufaa, tiba za asili zilikuwepo na ziliwasaidia wananchi wengi,” amesema Dkt. Eyembe.

Amesema uamuzi wa Serikali kuunganisha wataalamu wa afya na watoa tiba asili ni hatua muhimu itakayosaidia kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa salama, bora na zenye manufaa kwa wananchi wengi zaidi.

“Faida yake ni kubwa sana. Tukifanikiwa kufanya hivi, wananchi watapata huduma bora zaidi, gharama za dawa zitapungua na mfumo wa afya utaimarika zaidi,” ameongeza.

Dkt. Eyembe amesema hatua hiyo pia itasaidia kutambua rasmi mchango wa watoa tiba asili ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitoa huduma muhimu katika jamii, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia utaratibu unaotambulika kitaalamu.

“Tunachotaka ni kuona watibu wa asili wakifanya kazi kwa utaratibu unaotambulika huku wakishirikiana na wataalamu wa afya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Aidha, amesema ushirikiano huo utaongeza ufanisi wa huduma za rufaa kwa wagonjwa pamoja na kusaidia kuimarisha mfumo wa afya nchini.

Katika hotuba yake ya bajeti, Waziri Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kuratibu huduma jumuishi za tiba asili katika hospitali 14 za rufaa za mikoa nchini zikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora (Kitete), (Mbeya, Bombo, Sekou Toure, Singida, Simiyu, Temeke, Mwananyamala, Morogoro, Dodoma, Mt. Meru, Bukoba, Sumbawanga na Njombe) huku wagonjwa 648 wakipatiwa huduma hizo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026.

Aidha, jumla ya dawa 48 za tiba asili zimesajiliwa, huku dawa sita zikiendelea kufanyiwa tafiti za usalama na dawa mbili za kisukari zikifanyiwa utafiti wa ufanisi ili ziweze kutumika rasmi katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Miongoni mwa magonjwa yaliyotibiwa zaidi kupitia huduma hizo ni vidonda vya tumbo, pumu, maambukizi ya mfumo wa mkojo, bawasili, baridi yabisi, tezi dume pamoja na upungufu wa nguvu za kiume.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top