Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesisitiza kuwa mafanikio yake katika tafiti, ufundishaji na utoaji wa huduma kwa jamii yanategemea kwa kiasi kikubwa mchango wa wafanyakazi wake, huku kikiahidi kuendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na ustawi kazini.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa, amesema uongozi wa Chuo umejipanga kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na kuimarisha mazingira rafiki ya utendaji kazi.
Akijibu risala ya wafanyakazi, Prof. Muhairwa alieleza kuwa Menejimenti imepokea kwa uzito maoni, changamoto na mapendekezo yaliyowasilishwa, na itaendelea kuyafanyia kazi kupitia mifumo rasmi ya uongozi kwa lengo la kupata suluhisho endelevu.
Alibainisha kuwa SUA inaendelea kuboresha upatikanaji wa vitendea kazi kwa kuimarisha mifumo ya manunuzi na kushirikiana na wazabuni wenye uwezo wa kutoa huduma kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya taasisi.
Aidha, alikiri kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa ofisi, akieleza kuwa hali hiyo imetokana na ongezeko la watumishi ambapo jumla ya wafanyakazi 263 wameajiriwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita, huku 125 wakistaafu, hali iliyoongeza shinikizo la miundombinu ya ofisi.
Prof. Muhairwa alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano, uwajibikaji na maadili kazini, akihimiza utamaduni wa kuheshimiana miongoni mwa wafanyakazi kwa kauli mbiu: “Mkubwa amheshimu mdogo na mdogo amheshimu mkubwa.”
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa RAAWU tawi la SUA, Bw. Faraja Kamendu, pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi THTU tawi la SUA, Dkt. Nickson Mkiramweni, waliwasilisha risala ya wafanyakazi wakieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, huku wakisisitiza umuhimu wa mshikamano, heshima na ushirikiano kazini.
Viongozi hao walieleza kuwa wana imani na utayari wa Menejimenti katika kushughulikia hoja zilizowasilishwa, na kuwahimiza wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kulinda haki na maslahi yao kwa ufanisi zaidi.




