Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora , Mh. Ridhiwani Jakaya Kikwete alipokuwa anajibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti maalum Bi. Asha Juma Feruzi alipotaka kufahamu serikali imejipangaje kutatua tatizo la wahitimu wengi wa vyuo kukosa ajira kwa kuwa wamesoma kozi ambazo hazipo katika mfumo wa Ajira Nchini.
Mheshimiwa Waziri Kikwete amelihakikishia Bunge na mheshimiwa Mbunge Feruzi kuwa serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa changamoto iyo inatoweka kwa kuelekeza vyuo kushirikiana na wizara mama na Taasisi mbalimbali za serikali kuwasiliana kabla ya kupitishwa kwa Miundo ya Maendeleo ya Utumishi ya kada husika.
Akizungumza Bungeni, Mheshimiwa Waziri aligusia mfano wa hatua iliyofanywa na serikali na chuo cha Mzumbe Morogoro kutatua changamoto ya kada ya Maafisa wa Maendeleo ya Vijana.
