RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo amewaapisha viongozi mbalimbali walioteuliwa katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma, akiwataka kutanguliza maslahi ya wananchi na kufanya kazi kwa uadilifu, nidhamu na matokeo.
Miongoni mwa walioapishwa ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Evaline Wilbard Munisi, ambaye Rais amesema uteuzi wake umetokana na sifa, uwezo na uzoefu wake katika masuala ya umma.
"Evaline ni Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi; lakini nimeangalia wasifu wake, nikaona ana sifa za kuingia ndani ya Serikali na kutusaidia," amesema Rais Samia, akisisitiza umuhimu wa kuweka mbele maslahi ya Taifa bila kujali tofauti za kisiasa.
Rais amemtaka Dkt. Munisi kushirikiana kwa karibu na viongozi na watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu kusimamia haki na stahiki za wafanyakazi, pamoja na kuimarisha juhudi za kutafuta fursa za ajira, hususan kwa vijana ndani na nje ya nchi.
Aidha, Rais Samia amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Kheri Abdul Mahimbali, kuhakikisha taasisi hiyo inarejesha ufanisi na imani ya umma, hasa kufuatia changamoto zilizoainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
"Vyeo ni dhamana. Mungu amekuweka hapo ili utumikie watu," amesisitiza Rais Samia, akiwataka viongozi wote waliokula kiapo kutekeleza majukumu yao kwa unyenyekevu na uwajibikaji.
Viongozi wengine walioapishwa ni pamoja na Katibu wa Rais, Balozi Ali Jabir Mwadini; Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Communications Regulatory Authority, Mhandisi Peter Philip Mwasalyanda; Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Civil Aviation Authority, Dkt. Jabir Kuwe Bakari; pamoja na Mshauri wa Rais Masuala ya Jamii, Angela Charles Kizigha.







Comments
Post a Comment