MBUNGE wa Jimbo la Kasulu Vijijini Edibilly Kazala ameipongeza Serikali kupitia wizara ya Maji Kwa kutenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji mbalimbali, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Akizungumza Bungeni leo Mei 6, 2026 jijini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mbunge wa Kasulu Vijijini, Mhe. Edibilly Kazara ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa uamuzi wake wa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya miradi ya maji katika Jimbo la Kasulu Vijijini.
Hii ni hatua kubwa ya matumaini kwa wananchi wangu.” amesema
Ameongeza kuwa fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika vijiji vya Chekenya, Kablangiri, Muziwe, Nyakitonto, Malalo, Kazage, Makere, Nyangwa, Karimungoma, Rusesa pamoja na Kitye, sambamba na mradi wa Kizima unaotarajiwa kuchimbwa katika kijiji cha Chambugwe.
“Hakika hii ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuwaletea wananchi huduma ya maji safi na salama. Kwa niaba ya wananchi wa Kasulu Vijijini naishukuru sana Serikali kwa kuifikia wilaya yangu kwa vitendo,” amesema Mhe. Kazara.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kasi katika utekelezaji wa miradi hiyo akibainisha kuwa wananchi wa maeneo hayo wana kiu kubwa ya huduma ya maji.
“Naomba kusisitiza kwamba fedha hizi zitekelezwe kwa wakati ili wananchi wapate huduma haraka, kwani changamoto ya maji bado ni kubwa katika maeneo yetu,” ameongeza.
Aidha, ametaja changamoto ya upotevu wa maji nchini, akibainisha kuwa Taifa linapoteza zaidi ya asilimia 30 hadi 35 ya maji yanayozalishwa.
“Kati ya maji yote yanayozalishwa, sehemu kubwa inapotea kabla ya kumfikia mwananchi. Hii ni hasara kubwa kwa taifa letu,” amesema.
Ameishauri Serikali kuongeza matumizi ya Teknolojia za kisasa kama sensa za kugundua uvujaji wa maji pamoja na kuimarisha uwajibikaji wa watumishi wa ngazi za chini ili kudhibiti changamoto ndogo ndogo kabla hazijawa kubwa.
“Ni muhimu tukawa na mfumo madhubuti wa kushughulikia haraka uvujaji mdogo wa maji ili kuepusha hasara kubwa,” amesema.
Kwa mujibu wa takwimu alizozitaja, zaidi ya shilingi bilioni 185 hupotea kutokana na upotevu wa maji nchini, hali inayopunguza kasi ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe.Kazala ameunga mkono hoja ya bajeti na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha sekta ya maji nchini.
“Naunga mkono hoja na naishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika,” amesisitiza.



Comments
Post a Comment