MBUNGE wa Jimbo la Butiama, Mhe. Dkt. Charles Mahera ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya nchini kuanzia huduma za msingi hadi hospitali za rufaa.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya jana Mei 11, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Dkt. Mahera amesema Serikali imefanya mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya kupitia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
“Kabla sijasahau, kwa sababu ya utendaji mzuri wa Waziri wa Afya, ninaunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja,” amesema Dkt. Mahera.
Amesema mfumo wa huduma za afya nchini umeendelea kuimarika tangu mwaka 2021 baada ya Serikali kuongeza uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo, jambo lililowezesha wananchi wengi kupata huduma bora karibu na maeneo yao.
Dkt. Mahera amesema vifaa vya kisasa kama Digital X-Ray, Ultrasound na CT-Scan vilivyosambazwa katika hospitali mbalimbali vimeongeza ubora wa huduma za afya na kupunguza changamoto za rufaa.
Aidha, ameunga mkono mpango wa Serikali wa kujenga hospitali mpya ya kisasa ya Muhimbili akisema hatua hiyo itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za matibabu Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Tunataka Tanzania iwe sehemu ambayo wananchi wa nchi jirani watakuja kupata matibabu badala ya kwenda nje ya Afrika,” amesema.
Mbunge huyo pia ameipongeza Serikali kwa mpango wa kuanzisha viwanda vya dawa, vitendanishi na vifaa tiba akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza gharama za matibabu.
Katika mchango wake, Dkt. Mahera amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza zaidi katika huduma za afya ya msingi ili kupunguza msongamano katika hospitali kubwa za rufaa.
Amesema bado kuna upungufu wa watumishi wa afya pamoja na wataalamu wa kutumia vifaa tiba vya kisasa, hivyo akaomba Serikali kuongeza ajira katika sekta hiyo.
Pia ameishauri Serikali kuangalia maboresho ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili makundi mbalimbali yakiwemo bodaboda na mama lishe yaweze kunufaika na huduma hiyo muhimu.
Akizungumzia Jimbo la Butiama, Dkt. Mahera amesema kata tisa kati ya 15 bado hazina vituo vya afya, hivyo akaomba Serikali kuongeza uwekezaji katika maeneo hayo ili wananchi wapate huduma karibu zaidi.
“Uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya ni wa mfano na unahitaji kupongezwa,” amesisitiza Dkt. Mahera.


