MWANZILISHI wa Kidoti Foundation, Jokate Mwegelo, ameendelea kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuinua elimu ya sayansi nchini baada ya kufanikisha ziara ya wanafunzi 110 wa masomo ya sayansi kutoka Shule ya Sekondari Jokate Mwegelo, Kisarawe mkoani Pwani, waliotembelea STEM Park jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo imekuwa daraja muhimu la kuwaunganisha wanafunzi na ulimwengu halisi wa teknolojia, ikilenga kuwapa uzoefu wa moja kwa moja nje ya darasa. Kupitia mpango huo, wanafunzi wamepata fursa ya kuona, kugusa na kujifunza kwa vitendo dhana za kisayansi, jambo linalochochea uelewa wa kina, ubunifu na ari ya kujifunza zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Jokate amesema kuwa lengo kuu la Kidoti Foundation ni kuhakikisha vijana wanapata elimu inayogusa uhalisia wa maisha ya sasa, hususan katika nyanja za sayansi na teknolojia.
Ameeleza kuwa kuwapeleka wanafunzi katika mazingira kama hayo ni njia bora ya kuwajengea uwezo wa kufikiri kwa ubunifu na kutatua changamoto kwa kutumia maarifa ya vitendo.
“Katika dunia ya leo inayotawaliwa na teknolojia, ni muhimu kwa vijana wetu kupewa nafasi ya kujifunza kwa vitendo ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali,” amesisitiza Jokate.
Hatua hiyo inaakisi mchango mkubwa wa taasisi binafsi katika kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza elimu ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Pia inaibua matumaini mapya kwa wanafunzi, ikiweka msingi imara wa kizazi chenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana kimataifa.










