Na Mwandishi wetu Jovina Massano.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kupitia Kituo chake cha Mwanza inaendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda rasilimali za wanyamapori.
Akizungumza na Mwandishi wetu Mhifadhi wa Wanyamapori kutoka TAWA Kituo cha Mwanza,Bw.Omary Mhando,ameeleza kuwa elimu hiyo imelenga kuongeza uelewa mpana wa wananchi kuhusu masuala ya uhifadhi.
"Jamii ina wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi wanyamapori na makazi yao ili kuondokana na migogoro",amesema Mhando.
Aidha elimu hii inatoa fursa kwa wananchi na viongozi wa maeneo mbalimbali, kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa kina kuhusu masuala ya uhifadhi.
Ushirikiano huu umeleta mwitikio chanya kutoka kwa jamii,ambapo wananchi wameipongeza TAWA kwa jitihada hizo na kuomba elimu hiyo iendelee kutolewa mara kwa mara ili kuimarisha uelewa na ushiriki wao katika uhifadhi.
Katika hatua nyingine, Bw.Mhando ameutaarifu umma kuhusu uwepo wa duka la nyara katika Kituo cha Mwanza ikiwemo na kutoa maelezo kuhusu taratibu halali za umiliki wa nyara.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa katika usimamizi na uhifadhi bora.
TAWA inaendelea kusisitiza kuwa ushiriki wa jamii kwa kuwa ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uhifadhi endelevu wa rasilimali za wanyamapori kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.




