Handeni wajipanga kupokea wanafunzi wa elimu ya Amali

GEORGE MARATO TV
0

 


Na Mashaka Mhando, Mkata

HALMASHAURI ya Wilaya ya Handeni imetangaza mpango mkakati wa kukabiliana na ongezeko la kihistoria la wanafunzi wa kidato cha kwanza unaotarajiwa mwaka 2028, huku Jeshi la Polisi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wakitakiwa kuimarisha usalama wa miundombinu.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika Leo Aprili 30, 2026, katika ukumbi wa Mbweni Mkata, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Saitoti Stephen, amesema mwaka 2028 utashuhudia changamoto ya kipekee ya kimfumo.




Msongamano wa Wahitimu 2027

Saitoti amefafanua kuwa mabadiliko ya mtaala wa elimu yatasababisha makundi mawili ya wahitimu kwa mwaka 2027; kundi la darasa la saba (mfumo wa zamani) na darasa la sita (mfumo mpya). Hali hiyo inazua hitaji la dharura la upanuzi wa miundombinu ya shule ili kupokea 'Double Intake' hiyo.

"Tunapaswa kuanza maandalizi ya miundombinu ya vyumba vya madarasa na samani sasa kupitia Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC), ili kuepuka msongamano na kuhakikisha haki ya elimu kwa kila mwanafunzi inatimizwa bila kikwazo," alisisitiza Saitoti.


Miundombinu na Usalama Barabarani

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Amiri Ramadhani Changogo, ametoa agizo kwa Wakala wa Barabara (TARURA) kuboresha barabara mbadala ili kupunguza vifo na ajali za watembea kwa miguu katika barabara kuu ya Chalinze–Segera.

Changogo amebainisha kuwa barabara nyingi za vijijini zimeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha, hivyo kuitaka TARURA kufanya matengenezo ya dharura ili kurejesha mawasiliano ya kiuchumi kati ya vijiji na masoko.


Usimamizi wa Ilani na Kero za Wananchi

Mwenyekiti huyo amehitimisha kwa kutoa wito kwa madiwani wa wilaya hiyo kuwa chachu ya mabadiliko kwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030.

Amewataka madiwani kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawe mstari wa mbele kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.


"Dhamira ya chama ni kuona changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Madiwani lazima muwe daraja madhubuti kati ya wananchi na uongozi wa halmashauri kupitia uwajibikaji na uadilifu," alisema Changogo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top