MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Ghati Zephania Chomete, ameiomba Serikali kuharakisha utoaji wa fedha ili kukamilisha miradi ya maji mkoani Mara, akisema ucheleweshaji wa miradi hiyo unaendelea kuwaumiza wananchi, hasa wanawake wanaobeba mzigo wa kutafuta maji kila siku.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni Dodoma leo Mei 6, 2026, Mhe. Chomete amepongeza uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa dhamira yake ya “kumtua mwanamke ndoo kichwani” inaendelea kuonekana kwa vitendo.
Mhe. Chomete amesema licha ya Mkoa wa Mara kunufaika na miradi 77 ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 265 pamoja na miradi sita mipya, changamoto kubwa imebaki kuwa kutokukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati.
“Mhe. Waziri Aweso,wananchi wanahitaji majibu ya lini miradi hii itakamilika. Mradi wa maji wa Mji wa Isenye uliosainiwa tangu mwaka 2020 kwa zaidi ya shilingi bilioni 38 hadi sasa uko takribani asilimia 15 tu. Hii siyo hali ya kuridhisha,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa wanawake wa Wilaya za Rorya, Tarime Mjini, Tarime Vijijini na Serengeti wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma ya maji safi na salama, huku baadhi ya miradi ikiwa imesimama kutokana na changamoto za kifedha.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chomete amepongeza utekelezaji wa mradi wa Mgango–Kiyabakari uliogharimu takribani shilingi bilioni 7, lakini akaomba Serikali kushughulikia changamoto ya mabomba katika Kata ya Tegeruka ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo muhimu.
Amesisitiza kuwa dhamira njema ya Serikali itakuwa na maana zaidi endapo miradi ya maji itakamilika kwa wakati, ili kweli kumtua mwanamke wa Kitanzania mzigo wa ndoo kichwani na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.



Comments
Post a Comment