_▪︎ Aagiza TANROADS kumpata mkandarasi ndani ya wiki mbili_
_▪︎ Aelekeza fedha za awali zitolewe mara moja kuanza ujenzi_
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kuanza mara moja ujenzi wa barabara za Nyololo–Mtwango (km 40) na Mafinga–Mgololo katika Jimbo la Mufindi Kusini, mkoani Iringa, akisisitiza kuwa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ni maelekezo ya moja kwa moja yanayopaswa kutekelezwa bila kuchelewa.
Ameyasema hayo leo Jumamosi, Mei 2, 2026, alipofanya ziara ya kikazi katika Jimbo hilo na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Igowole, kata ya Igowole, ambapo pia alisikiliza kero na mahitaji mbalimbali ya wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Nchemba amesema Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo na kuleta matokeo kwa wananchi.
“Mheshimiwa Rais amejitambulisha kwa kazi zake kwamba yeye ni mtu wa matokeo,” amesema.
Katika hatua ya kuharakisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu, Waziri Mkuu ameagiza kuanza mara moja kwa ujenzi wa barabara hizo na kusisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa ahadi za Rais.
Akijibu hoja kuhusu barabara ya Nyololo–Mtwango, ameielekeza TANROADS Mkoa wa Iringa kuhakikisha mkandarasi anapatikana ndani ya wiki mbili ili kazi ianze mara moja.
“Sitaki majibizano ya barua ya vibali kwenye jambo ambalo Rais ameelekeza… tafuteni mkandarasi, ndani ya wiki mbili mniambie mmempata mkandarasi,” amesema.
Aidha, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo, akisisitiza kuwa ahadi ya Rais ni ya kutekelezwa kwa ukamilifu wake.
“Ahadi ya Rais mnajengaje mita 200, 200?” amesema.
Kuhusu barabara ya Mafinga–Mgololo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuandika barua mara moja kwenda Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupatiwa fedha za malipo ya awali ili mradi huo uanze bila kuchelewa.
“Andikeni barua leo leo, pelekeni Wizara ya Fedha kupewa advance payment… na nakala nileteeni ofisini kwangu Jumatatu niione. Mradi huu uanze mara moja,” amesema.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu pia alisikiliza kero mbalimbali za wananchi, ikiwemo madai ya malipo dhidi ya kampuni ya Leshenia Investment inayodaiwa kutowalipa baadhi ya wananchi waliotoa huduma au kufanya biashara nayo.
Akizungumzia suala hilo, amesema Serikali haitavumilia vitendo vya kunyanyasa wananchi na kuchelewesha haki zao.
“Nachukia sana unyang’anyi wa haki za watu… malipo ya hawa vijana wanaodai huko viwandani na kwenye kampuni hiyo yalipwe mara moja. Mkuu wa Mkoa simamia hili mara moja,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wadaiwa watakaokaidi maagizo hayo.
“Mkuu wa Mkoa na RPC watafuteni, wajisalimishe, wasipojisalimisha wakamateni… ninaporudi nataka nikute wamelipa,” amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali ipo kulinda haki za wananchi na haitaruhusu mtu yeyote kunyimwa malipo yake halali.
Awali, Waziri Mkuu alipita katika Kijiji cha Idofi, Mji wa Makambako, mkoani Njombe, ambapo aliwasalimia wananchi na kupokea taarifa kuhusu mradi wa umwagiliaji pamoja na soko la mbogamboga, sambamba na kusikiliza changamoto za wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, amesema changamoto ya barabara imekuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli za kiuchumi, hususan kwa wakulima kusafirisha mazao yao na viwanda kupata malighafi kwa wakati.








