Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

Diaspora Waongeza Uwekezaji Hadi Billion 11.7 Nchini


Serikali imefanikiwa kuimarisha ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) katika uchumi wa taifa, baada ya kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 11.7 kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS hadi Februari 2026, kutoka shilingi bilioni 7.5 zilizowekezwa mwaka uliopita.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi Leo Mei 26,2026 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ametoa Takwimu hizo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, zikionesha ongezeko la imani ya diaspora katika mifumo rasmi ya uwekezaji nchini.


Balozi Kombo ameeleza kuwa ongezeko hilo linatokana na jitihada za kimkakati za kuhamasisha taasisi za kifedha kutoa huduma mahsusi kwa Watanzania wa diaspora, lengo likiwa ni kuongeza ushiriki wao katika maendeleo endelevu ya taifa.

Katika hatua hiyo, akaunti maalum za diaspora zimeanzishwa katika benki sita ambazo ni TCB, CRDB, NBC, NMB, Azania na Absa, hatua inayorahisisha uwekezaji, utunzaji wa fedha na uhawilishaji wa fedha kutoka nje ya nchi kwenda Tanzania.

Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa diaspora wamewekeza zaidi kupitia ununuzi wa nyumba na viwanja vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.1 kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na taasisi nyingine, hali inayoonesha mwitikio chanya na dhamira yao ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Comments