MBUNGE wa Rorya, Mhe. Jafari Wambura Chege, ameibana Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Mkoa wa Mara, akieleza kuwa ni kinaya kwa mkoa huo uliobarikiwa na rasilimali kubwa ya maji kuendelea kukumbwa na uhaba mkubwa wa huduma hiyo muhimu.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji leo Mei 6, 2026, Bungeni Jijini Dodoma, Mhe. Chege amesema Takwimu zinaonesha Mara ni miongoni mwa mikoa ya mwisho kwa upatikanaji wa maji safi na salama, licha ya kuzungukwa na maji ya Ziwa Victoria kwa zaidi ya asilimia 70.
“Mheshimiwa Waziri, huu ni mkoa unaozungukwa na maji kwa zaidi ya asilimia 70, lakini wananchi wake bado wanateseka kutafuta maji. Hili halikubaliki,” amesisitiza
Amesema miradi mingi ya maji iliyoanzishwa imekwama na kushindwa kutoa huduma, hali inayosababisha malalamiko makubwa kwa wananchi, huku fedha nyingi zikiwa tayari zimetumika.
“Fedha zimetumika, lakini miradi mingi imesimama. Tunakuomba ufanye ziara maalum ukague na kuchukua hatua,” ameeleza.
Mbunge huyo pia amempongeza Waziri wa Maji kwa juhudi zake za kusukuma miradi mikubwa ikiwemo wa Nyashimo, lakini akasisitiza kuwa bado unahitaji nguvu zaidi za kifedha ili kumaliza kabisa tatizo la maji mkoani humo.
Katika hoja nyingine, Mhe.Chege ameibua mradi wa Nyarahara uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 160 lakini umekwama kutokana na upungufu wa shilingi milioni 20 pekee kwa ajili ya umeme, akieleza kuwa hali hiyo haiwezi kuvumilika.
“Wananchi wa zaidi ya kata 20 wanakosa maji kwa sababu ya milioni 20 tu. Hii ni fedha ndogo sana kulinganisha na mateso wanayopitia wananchi,” amesema.
Aidha, amekosoa urasimu katika ununuzi wa umeme kwa miradi ya maji vijijini, akisema mchakato mrefu unasababisha wananchi kukosa huduma hata kwa kiasi kidogo cha fedha.
“Haiwezekani wananchi wakose maji kwa sababu ya shilingi elfu 20 ya luku. Mfumo huu lazima urekebishwe haraka,” amesisitiza.
Ameishauri Serikali kuchukua hatua za haraka ili kukamilisha miradi hiyo na kuondoa kabisa changamoto ya maji, akisisitiza kuwa ndoto ya Serikali ya “kumtua mama ndoo kichwani” haiwezi kufikiwa bila utekelezaji wa vitendo.





Comments
Post a Comment