MBUNGE wa Jimbo la Butiama, Mhe. Dkt. Charles Mahera, ameiiomba Serikali kuharakisha uwekaji wa taa za barabarani katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo yanayopitiwa na barabara ya Mkutano,Natta kupitia Nyamwisuwa.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma Mei 26, 2026 wakati akiuliza swali la nyongeza, Dkt. Mahera amesema barabara hiyo ilianza kujengwa muda mrefu huku kipande cha Mkutano hadi Nyamwisuwa kikikamilika tangu mwaka 2007, lakini wananchi bado hawajanufaika na huduma ya taa za barabarani.
“Barabara hii inapitia maeneo mengi sana ya Jimbo la Butiama lakini maeneo hayo hayana taa kuanzia Nyambange, Nyakanga, Butuguri, Mbusegwe, Kiguri, Kiarano hadi Bisale. Wananchi wa Butiama wanasubiri taa hizi kwa muda mrefu tangu mwaka 2023,” amesema Dkt. Mahera.
Dkt. Mahera ameiomba Serikali kuhakikisha wananchi wa Butiama wanapatiwa huduma hiyo muhimu ili kuongeza usalama pamoja na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha miradi mipya ya barabara za lami inaenda sambamba na uwekaji wa taa za barabarani.
“Kwa sasa utaratibu wetu kila tunapojenga barabara, hasa za lami, tunaweka pia taa kwenye package ya mradi. Na kwa barabara zilizojengwa zamani sasa tunarudi kuhakikisha katika kila centre na maeneo yenye shughuli za biashara tunaweka taa,” amesema Kasekenya.
Amesema Serikali itahakikisha maeneo yote yaliyotajwa na mbunge huyo yanapatiwa taa za barabarani kulingana na mahitaji na shughuli zinazofanyika katika maeneo hayo.


Comments
Post a Comment