_▪︎ Asema hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma_
_▪︎ Aelekeza vituo vyote vitambuliwe na kuimarishwa_
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katika jamii, akisisitiza kuwa kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum si hisani bali ni wajibu wa pamoja wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo Aprili 6, 2026, alipojumuika na watoto wenye mahitaji maalum katika chakula cha pamoja kilichoandaliwa katika makazi yake ya Oysterbay jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Pasaka.
“Kufanya tukio la aina hii si hisani bali ni wajibu kama ambavyo hata maandiko matakatifu yanatutaka kufanya hivyo kuwahudumia wenye uhitaji,” amesema.
Amesema Pasaka ni fursa ya kuenzi na kuendeleza matendo ya upendo, huruma na mshikamano kwa vitendo, huku akiwahimiza Watanzania kuendeleza maadili hayo katika maisha ya kila siku.
“Leo tunapata fursa ya kutafakari kwa kina juu ya wajibu wetu wa kuendeleza matendo ya huruma, upendo na mshikamano katika jamii yetu,” amesema.
Aidha, amewatia moyo watoto hao kwa kusisitiza kuwa kila mmoja ana thamani na nafasi ya kufikia mafanikio bila kujali mazingira anayokulia.
“Watoto wote ni watoto wa Mungu… hakuna aliyewahi kuomba azaliwe wapi. Kila mmoja ana hatima yake,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameitaka Serikali kupitia wizara husika kuhakikisha vituo vyote vya kulea watoto vinatambuliwa na kurasimishwa ili viweze kusaidiwa ipasavyo.
“Tuendelee kufanya tathmini tuvijue vituo vyote vilivyopo ndani ya nchi yetu tuvirasimishe, na tusisubiri watu kutoka mataifa mengine kulea watoto wa nchi yetu. Lazima kila Mtanzania aone tuna wajibu wa watoto wetu,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wadau na jamii kuendelea kushirikiana katika kuwalea watoto hao kwa upendo, akibainisha kuwa jukumu hilo linahitaji moyo wa huruma na kujitoa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Maryprisca Winfried Mahundi, amesema Serikali itaendelea kuhimiza jamii kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na salama.
“Malezi bora yanahitaji zaidi ya chakula, mavazi na malazi yanahitaji pia uwepo wa mlezi anayemsikiliza mtoto, kumlinda dhidi ya ukatili na kumjengea mazingira ya kujiamini,” amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wote wanapata malezi bora na fursa sawa za maendeleo bila ubaguzi.













