WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa tasnia ya mazao ya bustani siyo tu sehemu ya sekta ya kilimo, bali ni sekta ya kimkakati ya biashara ya kimataifa inayounganisha Tanzania na Masoko ya Dunia.
Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ya Tanzania imeendelea kutoa ruzuku ya pembejeo iliyosaidia kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya bustani kutoka tani milioni 7. 5 kwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani milioni 9. 7 kwa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 30.2.
Amesema hayo leo (Jumatano, Aprili 22, 2026) alipozindua maandalizi kuelekea Jukwaa la Hotikacha la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji (Hortilogistica Africa 2026) lenye lengo la kukuza biashara ya mazao ya bustani, hafla hiyo imefanyika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Jukwaa la Kilimo wa Dkt. John Samwel Malecela Nzuguni jijini Dodoma. Jukwaa hilo linatarajiwa kufanyika jijini Arusha, Novemba 08 hadi 10, Mwaka huu.
“Ni dhahiri kuwa wadau wote tukishirikiana katika kuendeleza tasnia hii, mchango wake utaendelea kuwa mkubwa sana kitaifa na katika uchumi wa dunia kwa ujumla”.-Amesema Dkt. Mwigulu
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha Tanzania inaendelea inakuwa Kitovu cha Biashara ya Mazao ya bustani Afrika na lango la Masoko ya Kimataifa, Serikali imeendelea kupanua wigo wa masoko ya Kimataifa ambapo kwa sasa mauzo ya parachichi, mbogamboga, maua na viungo vinavyozalishwa nchini yameongezeka kwa kasi hususan katika Masoko ya Ulaya na Mashariki ya Kati.
Amesema kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuimarisha viwanda vya kuongeza thamani, kuimarisha mifumo ya ubora na viwango na kuboresha miundombinu ya usafirishaji ambapo ndege ya mizigo inaendelea kutoa huduma katika maeneo mbalimbali
"Serikali imewekeza katika cold chain systems katika Viwanja vya Ndege vya KIA pamoja Mwanza ambapo huduma ya kuhifadhi bidhaa zinazoharibika haraka yakiwemo mazao ya bustani inaendelea kupatikana."
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wakulima nchini kuzingatia ubora na viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuleta ushindani wa bidhaa za Kitanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, “Biashara ni ubora, bidhaa ikiwa na ubora haiwezi kukosa soko”-Alisisitiza Dkt. Mwigulu
Kadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa Tanzania ni sehemu salama, yenye fursa na inayokua kwa kasi kwa uwekezaji katika sekta ya kilimo. “Ninatoa rai kwa sekta binafsi kuendelea kusonga mbele, Serikali ipo bega kwa bega na ninyi”
Mheshimiwa Waziri Mkuu aliongoza harambee iliyolenga kukusanya shilingi bilioni 2 katika awamu ya kwanza. Hata hivyo, kiasi kilichopatikana kilivuka lengo hilo na kufikia shilingi bilioni 2.59. Kwa ujumla, ifikapo mwezi Novemba, jumla ya shilingi bilioni 6 inatarajiwa kukusanywa.
Kwa Upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema kuwa Jukwaa la Hoticulture na biashara na uwekezaji linalofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika na nchini Tanzania, limekuja wakati muafaka ambapo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameazimia kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji na uuzaji wa mazao ya kilimo barani Afrika na duniani.
“Hapa nchini Tanzania, Jukwaa hili linalenga kuwakutanisha wazalishaji kutoka bara ya Afrika, wanunuzi na watoa huduma kutoka nchi mbalimbali duniani, tunajivunia kutumia nafasi hii kutekeleza kwa vitendo falsafa ya kuwa na usalama wa chakula sambamba na kufanya biashara ya chakula na wengine”











