Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Daniel Sillo (Mb) amehutubia Mkutano wa 5 wa Mabunge Wanachama wa Mtandao wa Kibunge wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM-PN) na kueleza kwamba Bunge la Tanzania linaunga mkono Azimio la kulipa Bunge la Kiarabu hadhi ya mwangalizi.
Mhe. Sillo ameyasema hayo leo, tarehe 15 Aprili 2026 wakati akimuwakilisha Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu kwenye Mkutano huo wa 5 wa NAM-PN uliofanyika katika Hoteli ya Hilton Istanbul
Bomonti, jijini Istanbul, nchini Uturuki na aliambatana na Mhe. Elibariki Kingu (Mb).
Katika azimio hilo, mabunge wanachama yametambua umuhimu wa msingi wa kuendeleza uhusiano na taasisi nyingine za kimataifa kama sehemu muhimu ya ujenzi wa kitaasisi na uendeshaji wenye ufanisi wa NAM-PN.
Aidha, azimio hilo limezingatia maombi rasmi yaliyowasilishwa na Bunge la Kiarabu ya kutaka kuwa na hadhi ya mwangalizi katika mtandao huo.
Kwa hatua hii, Bunge la Kiarabu sasa litashiriki vikao na shughuli za NAM-PN kama mwangalizi, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kibunge na kukuza malengo ya pamoja ya nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.
Uamuzi huu uliopitishwa na Mabunge wanachana ikiwemo Tanzania, unaonesha dhamira yetu ya kujenga madaraja ya ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za Kiarabu zilizo chini ya Bunge la Kiarabu.







Comments
Post a Comment