Mbunge Ghati Asisitiza Umuhimu wa Kuwa na Vyama Vya Ushirika Vyenye Nguvu

GEORGE MARATO TV
0

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Ghati Zephania Chomete, amesisitiza umuhimu wa kujenga vyama vya ushirika vyenye msingi wa uadilifu, uwazi na uwajibikaji ili kuchochea maendeleo ya wanachama na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza leo Jijini Dodoma katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Ushirika pamoja na Uzinduzi wa Kampeni ya Uadilifu katika Ushirika, Mhe. Chomete ambapo amemwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, amesema kuwa ushirika usiposimamiwa kwa misingi sahihi unakosa tija inayokusudiwa.

“Vyama vya ushirika vinapaswa kujengwa katika misingi ya uwazi na uadilifu, huku usimamizi thabiti ukiwa kipaumbele ili wanachama wanufaike ipasavyo,” amesema Mhe. Chomete.

Ameongeza kuwa pamoja na usimamizi mzuri, vyama hivyo vinapaswa kuwajengea wanachama uwezo kupitia mafunzo ya kisasa ya biashara, masoko na usimamizi wa fedha ili viweze kuendana na ushindani wa kiuchumi wa sasa.

“Ni muhimu kwa wanachama kupewa maarifa na stadi za kisasa zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuongeza tija,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chomete ameeleza kuwa maendeleo ya ushirika hayawezi kufikiwa bila uwekezaji katika viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao, akibainisha kuwa hilo ni daraja muhimu la kuinua kipato cha wanachama.

“Hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya ushirika bila kuangazia viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao yetu; hili ndilo chachu ya uchumi imara wa wanachama,” amefafanua.

Aidha, ameishauri serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa vyama vya ushirika, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa mitaji na mikopo nafuu ili viweze kujiendesha kwa ufanisi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Upatikanaji wa mitaji na mikopo nafuu ni nguzo muhimu kwa vyama vya ushirika kuimarika na kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top