MVUTANO mkubwa umeibuka katika jamii ya Wazanaki kufuatia kile kinachodaiwa kuwa ni kusimikwa kwa kiongozi wa kimila (Omwami) kinyume na mila na desturi za kabila hilo, hatua iliyozua hofu ya kuvunjika kwa mshikamano wa kijamii.
Kiongozi wa mila na desturi za Wazanaki, Omwami Mazila Marwa, ameibuka hadharani na kulaani vikali tukio hilo, akisisitiza kuwa utaratibu wa kumpata Omwami ni wa kurithi kutoka kwa mtangulizi, si kwa maamuzi ya ghafla au njama za kifamilia.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, Omwami huyo amesema yeye alirithi nafasi hiyo kutoka kwa baba yake mzazi, marehemu Edward Marwa Ihunyo, aliyefariki mwaka 2014, na kwamba utaratibu huo ndio unaotambulika rasmi katika mila za Kizanaki.
Kutokana na hali hiyo, ameiiomba Serikali iingilie kati haraka iwezekanavyo ili kudhibiti mgogoro huo na kuwachukulia hatua wote waliohusika na mchakato huo unaodaiwa kukiuka mila.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Butiama wameonyesha wasiwasi wao juu ya tukio hilo akiwemo Yohana Wandiba, mkazi wa kijiji cha Busegwe, amesema jamii ya Wazanaki inafahamu vyema taratibu za kumpata Omwami, hivyo kilichofanyika ni kinyume kabisa na utamaduni wao.
Kwa upande wake, Khamis Nyamsindika kutoka kijiji cha Kisamwene kata ya Butuguri, amesema taratibu za kimila zimekuwa zikifanyika katika makazi ya kichifu tangu enzi za mababu, na kubadilishwa kwake ghafla ni dharau kwa historia na misingi ya jamii hiyo.
Naye Amos Kongoro Imenyi, mkazi wa Busegwe, amekumbusha kuwa mgogoro kama huo uliwahi kutokea hapo awali na kutatuliwa kwa ushirikiano wa wazee wa mila, ambapo ilikubaliwa wazi kuwa Mwl. Mazila Marwa ndiye Omwami halali.
Kutokana na Mawazo ya Wananchi Serikali imeombwa kusimamia makubaliano ya kimila na kuhakikisha yanaendelea kuheshimiwa ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara katika jamii hiyo.
Mwisho.
















