CCM yamlipua Heche:'Uchumi sio maneno ya kisiasa, lete takwimu

GEORGE MARATO TV
0

 


Na,Saleh Lujuo-Dodoma

KATIBU wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi, amemshukia Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), John Heche, akimtaka kuacha kutoa kauli za uchumi zisizo na takwimu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo  April 7,2026 jijini Dodoma, Kihongosi amesema kuwa mjadala wa uchumi, hususani suala la mafuta, hauhitaji siasa za majukwaani bali unahitaji uhalisia unaoongozwa na Takwimu na uelewa wa kina.

Kwa msisitizo, Kihongosi Amesema kuwa kauli zisizo na uthibitisho zinaweza kupotosha umma na kuongeza hofu kwa wananchi, hasa katika kipindi ambacho gharama za maisha na bei ya mafuta vinajadiliwa kwa uzito mkubwa nchini.

“Uchumi haujadiliwi kwa hisia au siasa nyepesi. Ni eneo linalohitaji takwimu, uchambuzi na uelewa wa kina kabla ya kuzungumza,” amesisitiza.

Kadhalika, Ameongeza kuwa ni vyema kwa viongozi kutumia muda kujifunza na kufahamu hali halisi ya mambo kabla ya kujitokeza hadharani kutoa matamko yanayoweza kupotosha jamii.

Katika hatua nyingine, Kihongosi ameeleza kuwa CCM inaendelea kusimamia kwa karibu mwenendo wa sekta ya mafuta ili kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya athari za kupanda kwa bei.

Sambamba na hayo, Kihongosi amesema chama hicho kinaielekeza Wizara ya Nishati kuangalia uwezekano wa kurejesha ruzuku kwenye mafuta ili kupunguza makali ya gharama kwa wananchi.

"hatua hiyo inalenga kuleta unafuu wa maisha, mfano ni wa mwaka 2022 ambapo serikali iliwahi kutoa ruzuku na kusaidia kudhibiti bei za mafuta nchini". Amesema

Mbali na hilo, amesisitiza kuwa CCM inaielekeza Wizara ya Nishati kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika licha ya changamoto zilizopo duniani.

 "nishati ya mafuta ni mhimili muhimu katika kukuza uchumi, hususan katika sekta za viwanda na uzalishaji". Amesema

Kadhalika, Kihongosi amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuendelea kuwa kiungo muhimu katika uagizaji wa mafuta nchini, pamoja na kudhibiti vitendo vya hujuma vinavyoweza kuathiri upatikanaji wa nishati hiyo ambapo Ameonya baadhi ya wafanyabiashara wanaochepusha meli za mafuta na kuuza katika masoko mengine kwa lengo la kupata faida kubwa.


Kauli hiyo inakuja wakati mjadala wa kitaifa kuhusu mafuta na gharama za maisha ukiendelea kushika kasi, huku wanasiasa kutoka pande mbalimbali wakitoa mitazamo tofauti juu ya hali hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top