Bajeti ya Kimkakati Wizara ya Nishati

GEORGE MARATO TV
0


 DODOMA.

WIZARA ya Nishati imeomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.5 kwa ajili ya matumizi ya wizara ya hiyo na taasisi zake katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Hayo yameelezwa leo Aprili 22, 2026 na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma.

 Amesema kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 2.4 sawa na asilimia 97.5 ya bajeti yote ya wizara ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo huku shilingi bilioni 63 sawa na asilimia 2.5 ya bajeti ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

"Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lijadili na kuidhinisha Bajeti ya jumla ya Shilingi Trilioni Mbili, Bilioni Mia Tano Ishirini na Tano, Milioni Mia Nne na Moja, Mia Moja Ishirini na Tisa Elfu (Shilingi 2,525,401,129,000) kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa mwaka 2026/27". Ameomba

Kadhalika waziri Ndejembi Ametoa mchanganuo wa fedha hizo ambapo Shilingi Trilioni Mbili, Bilioni Mia Nne Sitini na Mbili, Milioni Mia Tatu Sitini na Nne, Mia Nane Thelathini na Sita Elfu (Shilingi 2,462,364,836,000) sawa na asilimia 97.5 ya Bajeti yote ya Wizara ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

Amesema Kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Sita na Mbili, Milioni Mia Nne Arobaini na Tisa, Mia Saba Thelathini na Tano Elfu (Shilingi 1,602,449,735,000) ni fedha za ndani, na Shilingi Bilioni Mia Nane Hamsini na Tisa, Milioni Mia Tisa Kumi na Tano, Mia Moja na Moja Elfu (Shilingi 859,915,101,000) ni fedha za nje.

Aidha, amesema Shilingi Bilioni Sitini na Tatu,Milioni Thelathini na Sita, Mia Mbili Tisini na Tatu Elfu (Shilingi 63,036,293,000) sawa na asilimia 2.5 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. 

"Kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni Hamsini na Mbili, Milioni Mia Tisa Thelathini na Tisa, Sabini na Tano Elfu (Shilingi 52,939,075,000) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) na Shilingi Bilioni Kumi, Milioni Tisini na Saba, Mia Mbili Kumi na Nane Elfu (Shilingi 10,097,218,000) ni kwa ajili ya Mishahara (PE) ya Watumishi wa Wizara na Taasisi ya PURA". Amesema

Sambamba na hayo, Mheshimiwa Ndejembi amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mafuta nchini licha ya changamoto za kimataifa zinazoathiri mnyororo wa usambazaji wa nishati hiyo ikiwemo vita inayoendelea katika Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa za mafuta ya petroli kwa uhakika.

"Sambamba na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme, nchi yetu pia imeendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli licha ya changamoto za kimataifa zilizotokana na vita baina ya Marekani, Israel na Iran," amesema Mhe. Ndejembi.

Amefafanua kuwa vita hiyo imesababisha athari kubwa katika usambazaji wa mafuta duniani, ikiwemo kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz ambao hupitisha zaidi ya asilimia 20 ya mafuta yote duniani, pamoja na kuathiri miundombinu ya uzalishaji na uhifadhi wa mafuta.

"Hali hii imeathiri kwa kiasi kikubwa nchi za Mashariki ya Kati ambako Tanzania inaagiza takribani asilimia 59 ya mafuta yake, huku asilimia 41 ikitoka India ambayo nayo hutegemea mafuta ghafi kutoka ukanda huo huo," ameongeza

Kutokana na hali hiyo, Waziri Ndejembi amesema Serikali imechukua hatua za haraka na za kimkakati ili kulinda usalama wa nishati nchini. Moja ya hatua hizo ni kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuagiza mafuta ya kutosha kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa soko la mafuta duniani na iko tayari kuchukua hatua zaidi kulingana na mabadiliko yatakayotokea.

Kwa upande wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini chini ya Mwenyekiti wake Subira Khamis Mgalu, wameishauri Serikali kuhakikisha kwamba inasambaza mawakala hadi maeneo ya vijijini ili kuwezesha upatikanaji rahisi wa nishati na kuondoa gharama za usafirishaji ambapo imesema Utekelezaji huo utachangia kwa kiasi kikubwa kuenea na matumizi ya nishati safi nchini.

"Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kusambaza na kuchochea matumizi ya nishati safi kwa wananchi bado kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa Nishati hiyo na gharama pia". Amesema 

Amesema Kamati imebaini kwamba vituo au mawakala wa kusambaza nishati safi nchini hawajenea maeneo ya vijijini hivyo hali hiyo huongeza gharama za usafiri kwa wananchi ambao wengi vipato vyao ni vya chini.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ya ulioanza mwaka 2024 hadi 2034 wenye lengo la kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top