Mkinga
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Mwaki Mwakanjila Mwaki, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya biashara haramu ya mihadarati mkoani hapa.
Hukumu hiyo imetolewa Machi 31, 2026, na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga, Mheshimiwa Aziz Hamis Mzee, katika shauri la jinai namba CC 03556/2026.
Hakimu Mzee amesema Mahakama imeridhika pasipo shaka na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, uliothibitisha kuwa mshtakiwa alijihusisha na usafirishaji wa dawa hizo kinyume cha sheria.
Mapema, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Kelvin Kisanga, aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ambayo inahatarisha nguvu kazi ya Taifa na usalama wa jamii. Kisanga alisisitiza kuwa Serikali haitasita kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote wanaojaribu kutumia mkoa wa Tanga kama mapito ya dawa za kulevya.
Akisoma hukumu hiyo, Mheshimiwa Hakimu Mzee amesisitiza kuwa adhabu hiyo ya miaka 30 jela inalenga kuonyesha msimamo wa vyombo vya dola katika kulinda sheria za nchi. "Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hili kwa mujibu wa sheria, hivyo mshtakiwa anahukumiwa kifungo hicho ili iwe onyo kwa wengine," alisema Hakimu.
Hukumu hiyo imepokelewa kama ushindi mkubwa katika operesheni za kudhibiti dawa za kulevya wilayani Mkinga, eneo ambalo kutokana na jiografia yake ya mpakani, limekuwa likitumiwa na baadhi ya watu wasio waaminifu kupitisha bidhaa haramu. Mahakama imewahakikishia wananchi kuwa itaendelea kusimamia haki na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya makosa ya aina hiyo ili kudumisha amani na utulivu.
Mwisho


