Na Kepteni Emanuel Ngonela Msata Pwani.
Zoezi la pamoja la medani 'Justfied Accord 2026' lililohusisha Kikosi Maalumu cha JWTZ na Kikosi cha Jeshi la Marekani cha Walinzi wa Taifa Nebraska limehitimishwa tarehe 12 Machi 2026 kata ya Msata, iliyopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani
Akifunga zoezi hilo Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi Meja Jenerali Said Nkambi alisema " Majeshi yetu yamejijengea heshima na uwezo mkubwa katika utekelezaji wa majukumu.
Jeshi la Marekani linaendeleza uhusiano kwa kubadilishana uzoefu hasa mbinu za medani, utoaji huduma tiba hali inayojenga mtazamo chanya wa wananchi kwa jeshi.
Zoezi la 'Justified Accord 2026' limefanyika kwa mafanikio na maandalizi ya zoezi lijalo yatakuwa mazuri zaidi baada ya tathmini ya zoezi kufanyika na kubaini mapungufu ambayo yamebainishwa na kufanyiwa kazi.
"Marekani ni mshirika wetu wa kimkakati na tunategemea majeshi yetu yataendelea kubadilishana uzoefu katika masuala ya sayansi na, teknolojia. " alisema Meja Jenerali Nkambi
Aidha, hafla ya ufungaji wa zoezi hilo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Kijeshi na Kiraia, akiwemo Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Andrew Lentz, Mkuu wa Kamandi ya Marekani Ulaya Kusini kazi Maalumu Afrika Meja Jeneral Craig Strong.
Zoezi hilo lililoanza tarehe 23 Februari 2026 hadi tarehe 13 Machi lililenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuvijengea uwezo Vikosi vya JWTZ katika kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo ya asili, Mafunzo ya kukabiliana na uhalifu wa kimtandao, pamoja na utoaji huduma tiba.
Pia, Jeshi la Marekani kupitia Kikosi cha Walinzi wa Taifa Nebraska ambao wanaongoza Wakala wa usimamizi wa huduma za dharura jimboni Nebraska (Nebraska Emergency Management Agency), kupitia Ubalozi wa Marekani nchini wamelipatia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania magari tisa ya huduma za dharura ili kuokoa watu wanaoathirika na majanga mbalimbali. Sambamba na hilo wametembelea Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo kujionea utoaji huduma tiba.
Zoezi la pamoja la 'Justified accord 2026' limefanyika likilenga kubadilishana uwezo kiutendaji kukabiliana na changamoto mbalimbali.


