Na Ada Ouko, Musoma.
JUMLA ya watoto 832,448 walio na umri chini ya miaka 10, Mkoani Mara wanatarajiwa kupata chanjo ya polio ya matone kupitia kampeni maalumu itakayofanyika kuanzia march 24 hadi 27 mwaka 2026, katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Hayo yamebainishwa march 17,2026 na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Zabron Masatu wakati akiendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa mkoa huo juu ya uelewa wa magonjwa 14 yanayozuilika kwa chanjo ukiwemo ugonjwa wa polio.
"Tunatarajia kuwa na kampeni ya chanjo ya polio ya matone ambayo tutaitoa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu Tamisemi na wadau wa maendeleo ambao tunafanya nao kazi hapa nchini..
"Kampeni hii itafanyika katika mikoa saba ya kanda ya ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora, Kampeni hii itaanza march 24-27 mwaka huu 2026"
Amesema kuwa kampeni ya chanjo ya polio itazinduliwa kitaifa katika mkoa wa Mwanza na Waziri wa afya Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa march 24 ,na kwamba mkoa wa Mara unatarajia kuwafikia watoto wapatao 832,448 walio na umri chini ya miaka kumi.
Zabron amesema kufuatia ugonjwa huo kuwa tishio duniani ikiwemo nchi ya Tanzania ambapo ilipata mgonjwa wa polio kwa mara ya mwisho mwaka 1996,Huku uthibitisho wa uwepo wa virusi vya ugonjwa huo katika sampuli ya maji taka kwenye mazingira zilizokusanywa wakati wa ufuatiliaji wa kawaida Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ofisi ya waziri mkuu Tamisemi, na wadau imepanga kutekeleza utoaji wa chanjo hiyo ya polio kwa njia ya matone kwa watoto.
"Katika ufuatiliaji wa kawaida ambao umefanyika kuna virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio vimepatikana kwenye majitaka kule kwenye mkoa wa Mwanza, Ingawa mpaka sasa hakuna kirusi kilichopatikana kwa binadamu, lakini tumekipata mazingira anamoishi Binadamu hivyo huweza kukipata ndio maana serikali imeona umuhimu wa kuleta kampeni hii" Amesema Zabron.
Aidha amesema jamii inapaswa kutambua ugonjwa wa polio kuwa unasababisha kupooza kwa viungo vya mwili , ulemavu wa kudumu na vifo kwa watoto ambapo virusi hivyo huingia mwilini kwa njia ya mdomo kwa kula au kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa virusi hivyo, virusi huongezeka ndani ya utumbo na hutolewa kwa njia ya haja kubwa Kinachoweza kusababisha maambukizi kwa mtu mwingine.
Amesema kuwa ugonjwa huo hauna tiba lakini huweza kuzuilika kwa kupata chanjo ya matone sambamba na chanjo ya sindano, ametaja viashiria vya ugonjwa huo kuwa mtoto kulemaa ghafla kwa kushindwa kutembea, kulegea kwa viungo,mtoto kushindwa kukaa wakati mwingine mtoto huchechemea, na kutoa wito kwa jamii katika kipindi cha kampeni watoto walio na dalili hizo ni vyema wakapelekwa katika vituo vya kutolea huduma ya afya.
Naye Mratibu wa chanjo hiyo mkoani hapa Flowina Muuzaje amesema kuwa kampeni hiyo itafanyika nyumba kwa nyumba na maeneo yaliyo na mkusanyiko wa watoto kama vile shuleni, kwenye nyumba za ibada, kwenye masoko lakini kutakuwa na utoaji wa alama maalumu kwenye vidole vya watoto watakaochanjwa na nyumba zote zitakazofikiwa na kampeni hiyo zitawekwa alama ilikuonyesha kuwa eneo hilo limekwisha hudumiwa.
"Kutakuwa na timu ya wachanjaji ambao watafika katika maeneo hayo, pia kutakuwa na timu za wahamasishaji kwenye ngazi ya jamii wahamasishaji hao ni wanajamii wenyewe, Ieleweke kila mtoto atakayechanjwa tutatunza taarifa zake kwa kuweka kumbukumbu"amesema Flowina.
Amesema kupatikana kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa polio mkoani Mwanza iligundulika february 2025 katika wilaya ya Nyamagana na baadaye virusi hivyo pia viligundulika Ilemela Desemba 2025, katika majitaka na kwamba hakuna binadamu anayedhaniwa kuwa na virusi hivyo.






