Wanu Akabidhi Vifaa Vya Tehama Vya Mamilioni Kwa Shule za Msingi na Sekondari

GEORGE MARATO TV
0


 SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imetoa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya jumla ya Sh. 769,390,000 kwa shule za msingi na sekondari 19 zilizopo katika mikoa tisa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Vifaa hivyo vinajumuisha madarasa janja, mbao janja, vishikwambi na kompyuta, ambavyo vinatarajiwa kuwezesha ujifunzaji kwa wanafunzi, hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia. Aidha, walimu watanufaika kwa kutumia mbinu bunifu za ufundishaji pamoja na mifumo ya kidijitali kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa ufanisi zaidi.




Hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo imefanyika leo Machi 30, 2026 jijini Dodoma, ambapo Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. *Wanu Hafidh Ameir*, alisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Amesema mageuzi hayo yanalenga kuboresha elimu kwa kuimarisha elimu ya lazima ya miaka 10, kuendeleza mkondo wa elimu ya amali, na kuimarisha mafunzo ya ualimu, hususan katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

“Leo tumegawa vifaa hivi; niombe visifungiwe kabatini. Vitunzeni na vitumike kwa muda mrefu ili viwanufaishe wanafunzi wengi zaidi,” amesisitiza Mhe. Wanu

Aidha Mhe. Wanu ameishukuru Lyra Organisation in Africa pamoja na wadau wengine wa sekta binafsi kwa mchango wao katika kuimarisha matumizi ya teknolojia katika elimu, akihimiza ushirikiano huo kuendelea ili kujenga mfumo wa elimu wa kisasa na jumuishi unaotumia teknolojia kwa ufanisi.

Hata hivyo amewataka walimu, wanafunzi na wadau wote kutumia na kutunza vifaa hivyo ipasavyo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuboresha elimu nchini kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.





Prof. Nombo amesema  kuwa lengo la pamoja kati ya Serikali na wadau ni kuendeleza elimu na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika elimu, hatua inayolenga kuboresha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.

Prof. Nombo amesisitiza kuwa ugawaji wa vifaa hivyo ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata nyenzo bora za kuwawezesha kumudu ujuzi wa kidijitali unaohitajika katika dunia ya sasa.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top