Vikundi vya Mawasiliano vya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) vimekutana ili kujenga uwezo na uelewa wa pamoja katika fani ya mawasiliano leo tarehe 02 Machi 2025, Mkutano uliofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr iliyopo mjini Unguja, Zanzibar.
Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Amri Salim Mwami amesema Mkutano huo utawajengea uwezo wa utendaji washiriki, na kusisitiza kuwa mawasiliano yanahitaji vifaa bora na mafunzo ili kuongeza weledi katika utendaji.
Meja Jenerali Mwami aliongeza kuwa nia ya Mkutano huo ni kuwa na muongozo mmoja ili kuwepo na uelewa wa pamoja kwa majeshi ya SADC.
Aidha, mshiriki kutoka nchini Botswana Brigedia Jenerali Meshack Mosime amesema mkutano huo umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi wanachama wa Jumuiya na kwa mshiriki mmoja mmoja hasa katika fani ya mawasiliano, lakini pia wamepata fursa ya kutalii na kuona uzuri wa Tanzania hasa kisiwa cha Zanzibar.
Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki kutoka Majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.




