KONDOA
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala kwa wananchi, hususan wanawake wajasiriamali nchini.
Kupitia mpango huo, UCSAF imegawa Majiko ya Gesi 50 Kwa wanawake Wajasiriamali katika wilaya ya Kondoa Kwa lengo la kupunguza matumizi ya mkaa na kuni ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakichangia uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kiafya.
Akizungumzia katika Hafla ya Ugawaji wa Mitungi Kwa Wanawake Wajasiriamali katika Wilaya ya Kondoa, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Ramadhan Hamis, amesema Mitungi hiyo ya Gesi iliyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano Kwa wote itawasaidia wanawake hao kufanya shughuli zao za uzalishaji kwa ufanisi zaidi, salama na kwa gharama nafuu.
“Hapo awali ilikuwa ni vigumu kwa wananchi kubadili mazoea. Lakini sasa elimu imeeleweka na matokeo yake yanaonekana lakini pia Wanawake wengi wameanza kuhamia kwenye nishati safi,” amesema.
Ameeleza kuwa hatua hiyo si tu inapunguza utegemezi wa kuni na mkaa, bali pia inalinda mazingira na kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mahusiano UCSAF, Celina Mwakabwale, amesema Mfuko wa Mawasiliano Kwa wote umekuwa ukigawa Mitungi ya Gesi kwa makundi mbalimbali na kwa wilaya ya Kondoa wametoa mitungi 50 ya gesi kwa wanawake wajasiriamali kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).
“Hii ni hatua ya kuhakikisha nishati safi inayafikia makundi yote nchini na bado tunaendelea kuyafikia makundi mengine Kwa kiendeleza mpango wa kugawa majiko ya gesi kwa wajasiriamali wanawake Lengo ni kukuza matumizi ya nishati safi, kuokoa mazingira, na kuboresha afya kwa kupunguza moshi wa kuni/mkaa". Amesema
Kwa wanawake walionufaika Kwa kupewa mitungi hiyo ya Gesi akiwemo khanifa Hussein amesema Zamani alikuwa akitumia muda mwingi kutafuta kuni,hivyo kutokana na kuwezeshwa kwa Mtungi wa Gesi na kupata Elimu kuhusu nishati safi ya kupikia hatotafuta tena kuni bali atatumia Gesi hiyo kama mkombozi wake.
"Moshi ulikuwa mwingi na afya ilikuwa hatarini. Sasa nitaenda kupikia kwa amani na haraka,” Amesisitiza
Naye Amina Boniphace na Fatuma Ally nao wanakiri kuwa majiko ya gesi yatakwenda kuongeza tija katika biashara zao na kuwapa muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
“Tutafanya kazi kwa ufanisi zaidi sasa. hii itatusaidia sana hata kuongeza kipato,”..wamesema
"Tunawaomba UCSAF waongeze juhudi ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na nishati safi". Wameongeza
Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni, sambamba na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kulinda afya za wananchi na mazingira ambapo Matumizi ya Nishati safi ya kupikia inatajwa kuwa sehemu ya juhudi za taifa za kuimarisha matumizi ya nishati endelevu, zenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kulinda rasilimali za asili kwa vizazi vya sasa na vijavyo.











