Nyansaho Awapa Tumaini Jipya Wananchi wa Tarime

GEORGE MARATO TV
0


>>Ni kuhusu barabara ya TANROADS iliyogeuka mashimo

NA MWANDISHI WETU, Tarime 

MAKAMU Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara, Dkt. Rhimo Nyansaho, amewapa matumani wakazi wa wilaya Tarime kuhusu matenegenezo ya barabara ya Tarime-Mogabiri ambayo imechimbika mashimo kwa muda mrefu sasa.

Ni barabara inayotumiwa na maelfu ya wasafiri wakiwemo watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti na magari ya biashara kati mji wa Tarime, Nyamongo na Serengeti.

Barabara hiyo ipo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), lakini imebaki kulalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu sasa wakiomba itengenezwe bila mafanikio. 

“Naona nilisemee jambo hii, uhakika ni kwamba barabara hii imewekwa kweye mpango wa matengenezo na mkandarasi alishapatikana,” Dkt. Nyansaho ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alisema Jumatatu iliyopita.

Dkt.  Nyansaho aliyasema hayo mjini Tarime wakati akitoa salamu za pole kwenye mazishi ya Frank Peter Zakaria (41), kijana wa mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa na Chifu wa Koo ya Watimbaru, Peter Zakaria.

Kwa mujibu wa Dkt Nyansaho, kinachosubiriwa kwa sasa ni mkandarasi wa barabara hiyo kulipwa fedha ili kazi ya kuitengeneza ianze.

Alisema barabara hiyo pamoja na ile ya Sanzate-Natta ambayo itaunganisha wilaya za Serengeti na Bunda kwa lami zimepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani Mara.

"Kwa sasa serikali imeipa barabara hii ya Tarime-Serengeti) na ile ya Bunda-Serengeti kipaumbele mbele,” alidokeza maelfu ya waombolezaji waliohudhuria msiba huo kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa huo.

Dkt. Nyansaho alibainisha kuwa wakandarasi wa kujenga barabara hizo wanatarajiwa kulipwa fedha kufikia mwisho wa mwezi huu.

"Uhakika uliopo ni kwamba wakandarasi watakuwa wamelipwa kabla ya mwisho wa mwezi huu (Machi),” alisema.

Alisisitiza kuwa barabara hizo ni muhimu kwa maendeleo ya mkoa wa Mara, na kwamba serikali imedhamiria kuzipatia ufumbuzi wa kuzifanya zipitike bila shida.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, anatarajiwa kufanya ziara katika mkoa wa Mara mwishoni mwa mwezi huu, ambapo pamoja na mambo mengine, atakagua barabara hizo, kwa mujibu wa Dkt. Nyansaho.

Awali, badhi ya wasemaji katika mazishi hayo waliitaja barabara hiyo ya Tarime-Mogabiri kama kero ya muda mrefu ambayo ina madhara makubwa ya kiuchumi, huku ikiweka maisha ya watu hatarini.

"Hii barabara Mhe.  Waziri Nyansaho ni mashimo tupu, inaumiza watu, inaharibu magari ya watu,” alisema mkazi wa mjini Tarime, Chacha Heche, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mara.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Fadhili Maganya, naye alizungumzia barabara hiyo na kuagiza mamlaka husika kuhakikisha inatengenezwa mara moja.“Mimi ni msaidizi wa Mhe. Rais, hatuwezi kwenda hivi,” alionya kiongozi huyo wa chama tawala - CCM.

Katika hatua nyingine, Waziri Nyansaho alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania kudumisha amani,  mshikamo na upendo kwa maendeleo na ustawi wa taifa.

“Amani ni jambo la muhimu sana, maendeleo yanategemea amani. Twendelee kudumisha amani bila kujali itidadi za vyama vyetu wala koo zetu,” alisisitiza Waziri huyo wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top