DODOMA
SERIKALI kupitia Taasisi ya Tiba ya Mifupa na ubongo (MOI) katika kipindi cha mwaka 2025 imefanikiwa kuanzisha huduma mpya 9 za kibobezi ikiwemo huduma ya upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde ambazo hapo awali ziliwalazimu wagonjwa kuzifuata nje ya Tanzania.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na ubongo (MOI) Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani alizowahidi Watanzani.
Balozi,Dkt. Mpoki amezitaja huduma zingine zikiwemo huduma za Upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu,Huduma ya kuchukua sampuli za vipimo kwa njia ya matundu,Huduma ya kuweka tiba simenti kwenye pingili za mgongo zilizovunjika,Huduma ya tiba ya maumivu (Pain clinic).
Huduma ya upasuaji rekebishi wa viungo vilivyopooza,Huduma ya upasuaji wa uvimbe na ubongo kwa kutumia teknolojia ya fluorescein,
Kuanza kwa wodi mpya za kisasa za premier kwa ajili ya wagonjwa maalum na wakimataifa ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa maalum na wakimataifa,Kuanza kwa mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao.
"PiaTaasisi ya MOI imeendelea kutoa huduma nyingine za kibingwa Bobezi na kupunguza rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi na huduma hizo ni Upasuaji na uchunguzi wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu,Upasuaji wa Nyonga na magoti". Amesema
"Matibabu ya kiharusi kwa kupitia mishipa mikubwa ya damu,Upasuaji wa kunyoosha mgongo uliopinda (Kibiongo),Kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua, Huduma ya maumivu sugu ya mgongo, Huduma ya wagonjwa maalum na wagonjwa wa kimataifa, wagonjwa wamehudumiwa kutoka mataifa ya Congo, Comoro, Uganda, South Sudan, Burundi na mataifa mengine nje ya bara la afrika". Ameongeza
Aidha, Balozi Dkt. Mpoki amesema Katika kipindi cha mwaka mmoja Taasisi ya MOI imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi wa
Ujenzi wa jengo jipya la kuonea wagonjwa wa nje (OPD), unaogharimu kiasi cha Tsh.13.8 bilioni kutoka serikali kuu na mapato ya ndani.
"Mradi huu ukikamilika utapunguza msongamano wa wagonjwa katika OPD ya sasa kwani zaidi ya wagonjwa 1500 wataweza kuhudumiwa kwa siku". Amesema
"Na utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia arobaini (40%)"..Ameongeza
Ikumbukwe kuwa Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba 2025, Taasisi ya Mifupa MOI imehudumia jumla ya wagonjwa 176,987 kama wagonjwa wa nje na wale wa dharura (OPD na EMD) ambapo Kwa upande wa wagonjwa wa ndani (IPD), jumla ya Wagonjwa 9,922 walihudumiwa.



