Na: Mwandishi Wetu, Pangani
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina deni la kuwaletea maendelea wananchi kutokana na imani kubwa waliyonayo wananchi kwa Chama hicho.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) wilaya ya Pangani, Nasri Mkalipa, Machi 27, 2026, katika ziara yake ya ujenzi wa Chama katika Kata za Bushiri na Masaika.
Mkalipa amesema CCM iliomba ridhaa kwa wananchi na wananchi wakaichagua wakiamini yale waliyoahidi yatafanyiwa kazi, hivyo Chama kitaisimamia serikali kuhakikisha ahadi zote zinatekelezwa.
"Ndugu vijana wenzangu, tuendelee kuiunga mkono CCM, na jukumu letu ni kuwapa wananchi maendeleo. Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wetu Jumaa Hamidu Aweso na wadiwami wote wanapambana kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa," amesema Mkalipa.
Sanjari na hilo, Mkalipa amehimiza umuhimu wa vijana kushawishi vijana wenzao kujiunga na CCM na wapate kadi za kieletroniki ili watambuliwe Chamani.
Aidha, Mkalipa amewahimiza vijana kujitokeza kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na serikali huku akiwakumbusha Pangani imefunguka sana, wasibaki nyuma.
Huu ni mwendelezo wa ziara Operesheni Samia chini ya Katibu wa UVCCM wilaya inayoendelea kwa siku tisa kutembea Kata 14 za wilaya hiyo kuhakikisha uhai wa Chama unaimarika zaidi.





