Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Ghati Zephania Chomete, ameshiriki ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyofanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) inayolenga kuimarisha sekta ya uvuvi nchini.
Ziara hiyo ilifanyika jana tarehe 13 Machi 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo wajumbe wa kamati walitembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa meli za uvuvi, ujenzi wa gati, ujenzi wa ghala la kuhifadhia samaki (cold storage), pamoja na mitambo ya kutengeneza barafu inayotumika katika shughuli za uvuvi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, aliishukuru Kamati ya Bunge kwa kuisimamia sekta ya uvuvi kwa karibu kupitia ushauri na maelekezo kwa Serikali, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kufufuka kwa shughuli za Shirika la TAFICO.
Aidha, Waziri huyo aliwapongeza watendaji wa miradi ya uvuvi kwa juhudi wanazozifanya katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Deodatus Mwanyika, alilipongeza Shirika la TAFICO kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya uvuvi na kuomba Serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika sekta hiyo muhimu inayowanufaisha wananchi wengi, wakiwemo wavuvi wadogo na wa kati.
Kamati hiyo pia imeahidi kuendelea kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya uvuvi kwa kuhakikisha mipango ya TAFICO inatekelezwa ipasavyo ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Katika ziara hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi alieleza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, ambapo baadhi ya meli za uvuvi tayari zimewasili nchini na nyingine zinatarajiwa kununuliwa ili kukamilisha mpango wa kuwa na jumla ya meli tano za uvuvi.





