Wizara ya Uchukuzi Kuchukua Hatua Kali Kuwalinda Wanafunzi

GEORGE MARATO TV
0


 DODOMA.

WAZIRI wa Uchukuzi Mhe. Prof Makame Mbarawa amekemea vikali vitendo vya baadhi ya madereva na makondakta kukiuka kanuni na taratibu kwa kushindwa kuwabeba wanafunzi wakati wakienda shule na kurejea majumbani kwa madai ya kibiashara,jambo ambalo limesababisha baadhi ya wanafunzi kukatisha Masomo.

Waziri Mbarawa amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kali na stahiki dhidi ya watu wote wanaokiuka taratibu na kanuni za usafiri, bila kujali nafasi zao.

Kauli hiyo ya Serikali imetokana na kuona moja ya picha ya video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Jangwani Jijini Dar es Salam Mariana Eric Mirindima akiwasilisha barua iliyobainisha vitendo vya baadhi ya madereva na makondakta kuwanyanyasa na kuwanyima wanafunzi usafiri kwa madai ya kibiashara. 

Barua hiyo imeeleza kwamba kunyimwa usafiri Kwa wanafunzi kunasababisha kuchelewa au kushindwa kufika shuleni, kuhatarisha usalama wao na kuathiri haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Katika tamko lake mbele ya waandishi wa habari leo February 04 mwaka huu 2026 Jijini Dodoma,Waziri huyo wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema kutokana na changamoto hiyo serikali imechukua hatua za haraka kukomesha vitendo hivyo na kuwaondolea kero hiyo wanafunzi.

"Nimeona video clip kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ambapo binti aliyejitambulisha kwa jina la Mariana Eric Mirindima ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari Jangwani akiwasilisha barua yake iliyoeleza changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanaotumia usafiri wa mabasi ya mijini, maarufu kama daladala". Amesema 

"Katika barua yake, Mwanafunzi Mariana ameeleza kwamba makondakta wamekuwa wakigoma kuwabeba wanafunzi kwa kisingizio cha kibiashara wakidai kuwa wanafunzi hawalipi nauli kamili". Amesema

"Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wanalazimika kusimama barabarani kwa muda mrefu wakisubiri usafiri, wanachelewa kufika shuleni, na wakati mwingine wanashindwa kabisa kufika shuleni". Amesema

"Hali hii inawatia hofu wanafunzi, inawachosha, na inaathiri masomo yao, pamoja na usalama wao kama watoto. Alieleza pia kuwa wanafunzi wanategemea sana daladala kama njia yao kuu ya usafiri, hivyo wanapoachwa njiani au kunyimwa huduma wanakuwa kwenye mazingira hatarishi, na kunyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu kwa usalama". Amesema

"Hivyo, mwanafunzi Mariana akaomba, kwa niaba ya wanafunzi wengine, Wizara yangu ichukue hatua stahiki dhidi ya vitendo wanavyofanyiwa wanafunzi na watoa huduma za daladala (Wamiliki, Madereva na Makondakta)". Amesema

"Kisha akamalizia kwa kusema anawasilisha barua hiyo akiwa na matumaini makubwa kwamba sauti ya wanafunzi itasikilizwa na itafanyiwa kazi". Ameongeza

Sambamba na Hayo Waziri Mbarawa amemshukuru Mwanafunzi huyo na mzazi wake aliyesimamia kwa ujasiri na Kwa uamuzi huu wa kupaza sauti na kutoa mrejesho kuhusu changamoto hii kupitia mitandao ya kijamii. 

"Kwa kufanya hivyo, kijana huyu na mzazi wake wametimiza wajibu wao wa msingi wa kuipa Serikali na Mamlaka zote husika mrejesho unaopaswa kufanyiwa kazi. Na kwa hakika sauti ya wanafunzi imesikilizwa na itafanyiwa kazi". Amesisitiza

Aidha, Waziri Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Kuhakikisha zoezi la kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu (makondakta) kwenye mabasi linafanywa kwa kasi katika miji yote Nchini, na kutoa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria kwa madereva na makondakta watakaobainika kuwanyanyasa wanafunzi.

"Wahakikishe kuimarisha udhibiti wa nauli maalumu za wanafunzi, staha ya huduma na usalama wao kwa wakati wote;Kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma, na watumia huduma wajue haki na wajibu wa kila mmoja;Kuhakikisha Treni za Abiria, Daladala zote Nchini pamoja na Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi jirani zimeandikwa namba za bure ili abiria waweze kupiga LATRA 0800 11 00 19 na 0800 11 00 20". Amesisitiza

 "LATRA Pia shirikisheni Jeshi la Polisi ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza kwenye vituo vya daladala hasa nyakati za asubuhi na jioni kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri". Ameongeza 

Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kuwa ni watoa huduma za usafiri wa abiria baina ya miji, mijini na vijijini, ikiwa ni pamoja na Daladala zinazotoa huduma mijini ikiwa ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa huduma hizi zinaimarika kila wakati kupitia jukumu walilopewa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kisheria. 



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top