Arusha, Februari 9, 2026
Mkutano wa siku mbili wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii, umeanza leo Februari 9, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano AICC jijini Arusha, ambapo Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii imezinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano na uzinduzi wa Sera hiyo, Mhe. Sangu alisema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliahadi kuwa na Sera hii, ambayo lengo lake ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma anapokumbwa na changamoto kama umaskini, uzee, ulemavu, magonjwa, ukosefu wa ajira, majanga ya asili.
Miongoni mwa wadau wakubwa wa Sekta ya Kinga ya Jamii wanaoshiriki katika mkutano huo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Akizungumzia mchango wa Mfuko huo katika utekelezaji wa Sera ya Kinga ya Jamii, Mhe. Sangu alisema, PSSSF imeweza kuongeza idadi ya wanachama kutoka 697,677 Juni 2020 hadi kufikia 889, 948, Desemba 2025.
Uwekezaji wa PSSSF nao umeongezeka kutoka trilioni 5.66 Juni 2020 hadi kufikia trilioni 10.51 Desemba 2025.
Aidha, thamani ya Mfuko wa PSSSF imeongezeka kutoka trilioni 5.74 Juni 20, 2020 hadi kufikia trilioni 12.96 Disemba 2025, alisema Mhe. Sangu.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, alisema PSSSF kama moja ya taasisi za kinga ya jamii, iko mstari wa mbele kutekeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na kuwahakikishia wanachama kuwa Mfuko uko imara na utaendelea kuwahudumia kwa uaminifu na kwa umahiri mkubwa.
Akizungumza hivi karibuni kwenye uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi PSSSF ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo alisema, katika kipindi cha Nusu Mwaka Julai-Disemba 2025, PSSSF ililiingiza katika mzunguko wa fedha kwa njia ya ulipaji wa mafao shilingi bilioni 883.



