Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Yaendelea Kuchangia Kasi ya Ukuaji wa Uchumi Nchini-Waziri Kairuki
DODOMA.
KATIKA kipindi cha siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kukua kwa kasi ikichangiwa na uwekezaji ulioendelea kufanywa na Serikali hususani kwenye ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo Minara na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Akielezea amafanikio hayo ya siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani Leo Feb 4,2026, waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angel Kairuki amesema upatikanaji wa Mawasiliano nchini unaendelea kuimarika.
Amesema mwenendo huo unaashiria kuendelea kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma za mawasiliano.
"Takwimu zinaonesha kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 99.3 Oktoba, 2025 hadi laini milioni 106.9 Januari, 2026 sawa na ongezeko la asilimia 7.7". Amesema
"Watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 56.3 Oktoba, 2025 hadi milioni 58.1 Januari, 2026 sawa na ongezeko la asilimia 3.2". Amesema
"Watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka pia kutoka milioni 71.7 Oktoba, 2025 hadi Milioni 76.5 Januari, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 6.7". Ameongeza
Aidha,Waziri Kairuki amesema upande wa gharama za mawasiliano, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kudhibiti ongezeko la gharama za mawasiliano ambapo gharama za kupiga simu ndani ya Nchi zimeendelea kuwa Shilingi 29 kwa dakika.
"Wastani wa bei ya Data bila kifurushi nayo imeendelea kubaki Shilingi 9.35 kwa kila MB 1 hadi". Amesema
"Mwenendo huu unaashiria kuendelea kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma za mawasiliano". Amesema
"Hatua hii imepelekea wananchi kufikiwa na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kidijitali kama vile huduma za Kifedha, afya, kwa urahisi na kwa haraka". Amesema
Sambamba na Hayo, Amesema katika kuhakikisha vijana Wabunifu Nchini wanakua na chanzo cha fedha chenye uhakika kukuza bunifu zao, serikali imeweka maandalizi na taratibu za uanzishwaji wa Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA (ICT Startups Development Fund).
"Mfuko huu utawezesha upatikanaji wa mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara kwa Kampuni Changa ambazo mara nyingi hazipati mtaji kutoka Benki na Taasisi nyingine za fedha au wawekezaji wa kawaida". Amesema
"Hatua hii pia ya uanzishwaji mfuko wa Kitaifa wa uwezeshaji wa Kampuni changa utakapokamilika, itawasaidia vijana kuanzisha biashara zao, kuboresha bidhaa/huduma wanazozitoa pamoja na kuwawezesha kufikia soko kwa haraka zaidi". Ameongeza
Pia,Amesema Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali imeweza kuunganisha Taasisi 800 za Umma kwenye Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali (GovNet).
Amesema hatua hiyo imerahisisha upatikanaji na matumizi ya mifumo ya TEHAMA ambayo imekuwa ikitumiwa na Wananchi kuwasilisha malalamiko yao kidijitali pamoja na viongozi wa Taasisi kutoa majibu na kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi.
"Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea na ukamilishaji wa utengenezaji wa Mfumo wa Tembo Portal, utakaotumiwa na Wananchi kuweka miadi (appointments) ya kukutana na viongozi wa Wizara (Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu) kwa lengo la kuwasilisha kero na changamoto zinazowakabili katika Sekta ya Mawasiliano na TEHAMA". Amesema
"Kwa sasa, mfumo huo upo katika hatua za majaribio, na utazinduliwa rasmi pamoja na mifumo mingine muhimu ikiwemo Jamii Portal Mwezi Aprili, 2026". Ameongeza
Ongezeko la huduma za Mawasiliano limechochea ukuaji wa uchumi wa watu na Taifa kwa ujumla hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imejikita katika kujenga uchumi wa kidijitali.




Comments
Post a Comment