Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limekifungia kiwanda cha HOOTA kilichoko Mkuranga Mkoa wa Pwani kutokana na kuchafua mazingira na kuhatarisha afya za wakazi wa eneo hilo.
Kiwanda hicho cha kurejeleza taka za plastiki kilichoko Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani kilifungwa jana na maofisa wa baraza hilo waliofika kiwandani hapo na kufanya ukaguzi.
Baada ya kufika kiwandani hapo maofisa wa NEMC walifanya ukaguzi na kujiridhisha kuwa kiwanda hicho kimeshindwa kuzingatia sheria ya mazingira kwa kushindwa kutibu majitaka yanayozalishwa.
Akizungumza mara baada ya kufunga kiwanda hicho, Meneja wa Utekelezaji wa Sheria wa (NEMC), Luvilo Mwamila alisema kiwanda hiko kiko kwenye makazi ya watu na kimekuwa kikitiririsha majitaka kwa wananchi na kuhatarisha afya zao.
Alisema kwa kawaida kiwanda hicho kinazalisha majitaka ambayo yanatakiwa kutibiwa kabla ya kwenda kwenye makazi ya watu lakini wamekuwa hawafanyi hivyo
Alisema mbali na majitaka hayo yenye viambata vya sumu pia kiwanda hicho kinazalisha hewa yenye kemikali ambayo pia inapaswa kudhibitiwa ili kulinda afya ya wafanyakazi na wananchi wengine jirani.
Alisema NEMC inaunga mkono uwekezaji lakini kiwanda hicho kinachangamoto nyingi ikiwemo kukosa cheti cha mazingira kwani hakikufanya tathmini ya athari kwa mazingira wakati wa kuanzishwa kwake.
“Kinatumia teknolojia ambayo haiwezi kudhibiti kemikali ambayo inazalishwa wanapoyeyusha taka za plastiki na wafanyakazi hawana vifaa kinga wakati wa kufanya kazi, NEMC ilishawapa maelezo wazingatie masharti hayo lakini hawajatekeleza,” alisema
“Tulishawaambia kuwa hapa walipojenga kiwanda ni makazi ya watu wahamie maeneo ya viwanda lakini wameshindwa kufanya hivyo. Aliomba miezi minne ili aweze kumalizia mzigo alionao lakini uchafuzi wa mazingira umezidi,” alisema Luvilo
Aidha, alisema NEMC ilimshauri ahamie eneo lisilo na makazi ya watu na kabla ya kuhamia awe amefanya tathmini ya athari kwa mazingira na kuweka teknolojia itakayodhibiti hewa ya kemikali isitoke nje na wadhibiti majitaka.
“Miezi minne aliyopewa ilipaswa kuisha mwezi wan ne mwaka huu lakini NEMCimegundua kuwa mwekezaji ameendelea kukiuka maelekezo kwasababu anaingiza mizigo mingine kiwandani kila siku na anaruhusu majitaka kwenda kwenye makazi ya watu,” alisema
“Tunakifungia kiwanda watafute eneo lingine ambalo ni sahini na wafanye tathmini ya mazingira na watumie teknolojia ya kisasa inayotunza mazingira,” alisema







