Musoma Mjini
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa, leo ametoa sadaka maalum kwa viongozi wa dini ya Kiislamu katika Misikiti tofauti ya Musoma Mjini ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono maandalizi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Sadaka hiyo imelenga kuwasaidia viongozi wa dini pamoja na waumini katika kujiandaa na mwezi huo muhimu wa ibada, unaoheshimiwa na Waislamu duniani kote. Baadhi ya vitu vilivyotolewa ni pamoja na buswati, tende, kanzu, balaghashee pamoja na fedha taslimu, ambavyo vimekabidhiwa kwa viongozi kutoka misikiti mbalimbali ya Musoma Mjini.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Agnes Marwa alisema kuwa sadaka hiyo ni ishara ya mshikamano, upendo na heshima kwa viongozi wa dini, pamoja na kuthamini mchango wao katika kujenga maadili mema na amani ndani ya jamii.
“Nimeona ni muhimu kushiriki na ndugu zetu wa Kiislamu katika maandalizi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Huu ni mwezi wa ibada, subira, na kusaidiana, hivyo ni wajibu wetu kama viongozi kuendelea kuwa karibu na jamii na kuunga mkono juhudi zao,” alisema Agnes Marwa.
Kwa upande wao, viongozi wa dini walipokea sadaka hiyo kwa shukrani kubwa, wakieleza kuwa msaada huo utasaidia katika maandalizi ya mwezi wa Ramadhani na kuimarisha zaidi mshikamano kati ya viongozi na jamii.
Hatua hiyo imepokelewa vyema na wananchi na waumini wa Dini ya kiislamu, wakieleza kuwa inaonyesha mfano wa uongozi unaojali na kuthamini imani, umoja na ustawi wa jamii ya Kitanzania.









