DODOMA
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 imetekeleza mpango mkakati wa kisayansi wa kujenga umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa Watoto wa Elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la pili ili kukabiliana na changamoto ya uwepo wa wanafunzi wanaohitimu Elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 31Januari, 2026, Waziri wa Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Mpango mkakati huo unaotekelezwa ndani ya miaka mitano unalenga kuhakikisha Kila mtoto anamudu stadi za Msingi afikapo darasa la tatu kupitia njia za kisayansi shirikishi na bunifu.
"Wataalamu wa elimu wameonesha wazi kuwa katika nchi yetu, ndani ya miaka minane ya mwanzo, watoto wetu huwa katika umri muafaka kabisa wa kujenga misingi ya mawasiliano na uelewa wa kusoma". Amesema
"Tunapojua kwamba mtoto huanza Darasa la Kwanza akiwa na umri wa miaka sita, Darasa la Pili miaka saba, na Darasa la Tatu miaka minane, ni dhahiri kuwa mkakati huu umejikita zaidi katika elimu ya awali, Darasa la Kwanza na Darasa la Pili, ili afikapo Darasa la Tatu mtoto awe tayari amepata mafanikio makubwa katika kusoma, kuandika na kuhesabu". Amesisitiza
Sambamba na Hayo, Prof Mkenda amesema katika siku 100 za Dkt. Samia Suluhu Hassan wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imeendelea kutekeleza Maboresho ya sera ya Elimu ujuzi pamoja na kuweka mkazo katika Masomo ya Sayansi na Teknolojia ili kupata vijana wenye uwezo mzuri.
Kadhalika,Serikali imesisitiza marufuku ya mwanafunzi kurudishwa nyumbani au kuadhibiwa kwa sababu ya michango, ikisisitiza kuwa tayari imetangaza elimu bila ada ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki ya msingi ya elimu.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amewataka wakuu wa shule kuzingatia kikamilifu kalenda ya masomo na ufundishaji inayotolewa na Kamishna wa Elimu, ili kuwapatia wanafunzi muda wa kupumzika, hususan katika vipindi vya likizo.
"Hatua hii inalenga kulinda haki za wanafunzi, kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ustawi wa mtoto na ubora wa elimu kwa ujumla". Amesema
Juhudi kubwa za serikali zimekusudia kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya msingi kwa kuondoa vikwazo kama vile ada na michango ili watoto wasome kwa bidii pasipo kikwazo chochote.






Comments
Post a Comment