Waandishi wa habari nchini wameaswa kutumia fursa ya ulimwengu wa kidijitali ikiwemo mitandao ya kijamii kujiajiri ili kupunguza tatizo la ajira nchini.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa mwanza Edwin Soko wakati akikabidhi Tuzo Mkurugenzi wa Bmg media George Binagi.
Tuzo hiyo imetolewa na Mtandao wa Youtoube baada ya chombo hicho cha habari za mtandaoni kufikisha idadi ya wachangiaji laki moja.
Soko amewaasa waandishi wa habari kuachana na kasumba ya kutaka kuajiriwa na badala yake wajiajiri kwenye ulimwengu wa kidijitali ambako kuna fursa nyingi zitakazoweza kuwakwamua kiuchumi.
‘’Tunapozungumzia Bmg tunazungumzia uchumi wa kidijitali,uchumi wa kidijitali kwa wale ambao mnaona ugumu kidogo ndio huu sasa,tutumie fursa hii kujiajiri na kutengeneza nafasi za ajira,zamani tulikuwa tunasema kama mjini pagumu shika Jembe ukalime,lakini siku hizi mabadiliko ya tabia nchi hata ukirudi kijijini mazao yatanyauka kutokana na ukame’’alisema Soko na kuongeza kuwa
‘’Fursa iliyobaki ni ya kidijitali,kwa hiyo George na Bmg kama Mkurugenzi Jaribu kuona kuna fursa kubwa ya kidijitali na uendelee kufanya hivyo na kwa sisi tulioshiriki hapa tuna wajibu vile vile wa kuishi katika mentality wa kutaka kuwa na shughuli zetu binafsi ambazo hazina limit na zinazoweza kutufanya kujiajiri zaidi’’alisema Soko.
Kwa mujibu wa Soko ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa afrika(Misa Tan), hatua ya mtandao wa kijamii wa BMG kufikisha wachangiaji laki moja si jambo dogo ambapo tuzo hiyo imetokana na kutambuliwa kwa mchango wake wa kimaadili kwenye uandishi wa habari.
Amemuasa Binagi kujiwekea malengo ya kukuza zaidi mtandao wake ikiwemo kuajiri wataalam zaidi ili kutimiza malengo yanayokusudiwa.
Kwa upande wake,Binagi akizungumza wakati wa hafla hiyo amesema kuwa Tuzo hiyo imemuongezea ari ya kujituma zaidi.
‘’Fursa hii inatuwezesha kupata riziki wakiwemo wale ambao wako nyuma yetu,kwa hiyo unaweza kuona jinsi ulimwengu wa kidijitali ulivyo fursa ya kiuchumi’’alisema Binagi
Binagi amewahiza vijana kuchangamkia fursa hiyo ili kukabiliana na changamoto ya ajira inayowakabili wengi wa wahitimu ya masomo ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma.
Ameziomba mamlaka zinazohusika kuendelea kuweka mazingira mazuri ili kuvutia vijana wengi zaidi kuwekeza kwenye ulimwengu wa kidijitali ikiwemo kupunguza ada ya usajili ya vyombo vya habari za mitandaoni kutoka shilingi laki tano ya sasa hadi laki moja .
Aidha ameiasa serikali kuwa walezi kwa vijana waliojiajiri kwenye ulimwengu wa kidijitali ikiwemo kutumia busara inapotokea changamoto ya maudhui mtandaoni badala ya kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika ikiwemo kutoza faini.
Pia Binagi ameomba serikali kuacha kutoza wazalishaji wa maudhui mtandaoni kodi mara mbili ikiwemo kodi ya mapato inayolipwa Mamlaka ya mapato pamoja na asilimia tano ya mapato yatokanayo na google.
Chombo cha habari cha mtandaoni cha Bmg kilianzishwa mwaka 2014 na ni miongoni mwa vyombo vya mwanzo kuanzishwa mkoani mwanza.


























Comments
Post a Comment