Ulinzi wa Msitu wa Mgori Kuimarika

GEORGE MARATO TV
0


TFS kuongeza askari, vifaa na kujenga kituo cha walinzi Pohama


Na Mwandishi Wetu, Singida

Ulinzi wa Msitu wa Hifadhi wa Mgori mkoani Singida unatarajiwa kuimarika baada ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, kutangaza mpango wa kuongeza askari, kupeleka vifaa vya kisasa vya ulinzi na kuanzisha ujenzi wa Ranger Post katika kijiji cha Pohama.

Profesa Silayo alitoa ahadi hiyo leo Jumanne, Novemba 11, 2025,  wakati wa kikao maalum cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Singida, kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mhe. Godwin Gondwe, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa Msitu wa Mgori.

Msitu huo, ambao ni miongoni mwa hifadhi muhimu nchini, umekuwa ukikabiliwa na changamoto za uchomaji moto, ukataji miti holela na uvamizi unaoathiri juhudi za Serikali katika kulinda rasilimali za misitu.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Gondwe alisisitiza umuhimu wa uhifadhi shirikishi, akipendekeza doria za pamoja kati ya TFS, Jeshi la Polisi na wananchi wa vijiji vinavyopakana na msitu huo. Pia alitaka kuboreshwa kwa miundombinu ya ulinzi katika eneo la Pohama lililoko mpakani mwa Wilaya ya Hanang’.

Akijibu hoja hizo, Profesa Silayo alisema TFS imejipanga kuongeza nguvu kazi na vifaa vya kisasa ili kudhibiti uharibifu wa misitu na kulinda rasilimali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Tutapeleka askari wa kutosha, vifaa vya ulinzi na kuanza ujenzi wa kituo cha walinzi Pohama ili kuhakikisha ulinzi wa Msitu wa Mgori unakuwa wa kudumu na endelevu,” alisema Profesa Silayo. 

Kamishna huyo pia aliishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa ushirikiano wao katika kusimamia hifadhi za misitu na nyuki, akisema juhudi za pamoja ndizo zinazowezesha mafanikio ya uhifadhi.

Akihitimisha kikao hicho, Mhe. Gondwe alimpongeza Profesa Silayo kwa mwitikio wa haraka na kwa uongozi unaolenga matokeo katika sekta ya uhifadhi.

“Tunathamini ushirikiano wa karibu kati ya TFS na Serikali za Mitaa. Msitu wa Mgori ni urithi wa taifa unaohitaji kulindwa kwa nguvu zote,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top