Na Mwandishi Wetu, Serengeti
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewaeleza wananchi wa Mkoa wa Mara kuwa, Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030, imebeba matumaini makubwa kupitia miradi ya maendeleo ambayo itafungua uchumi na kukuza uchumi.
Amesema miongoni mwa miradi mikubwa ambayo imeahidiwa na ilani kujengwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni bandari ya Musoma na uwanja wa ndege wa Serengeti.
Wasira ameeleza hayo leo Oktoba 17, 2025 katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
"Tunataka kujenga uchumi shirikishi na kuweka miundombinu itakayofanya uchumi ukue, moja tunajenga kiwanja cha ndege katika mji wa Mugumu, cha kisasa na kazi imeshaanza ya kufanya 'survey' ya kile kiwanja na kwenye ilani tumeyaandika, mimi mwenyewe nilikuwa mjumbe wa kamati iliyoandika ilani kwa hiyo nayajua.
"Musoma pale tunajenga bandari kama hatua ya kwanza ya kuunganisha bandari ya Musoma na bandari ya Tanga kwa ajili ya ujjenzi wa reli.
"Hapa Mugumu tunaunganisha barabara ya kutoka Tarime kuja Mugumu, maana nimekwenda Tarime pale kuna 'vindege' vinatua nikafikiri watalii wanakwenda Tarime, lakini kumbe shida yao ni kuja Serengeti.
"Sasa tutawajengea kiwanja hapa na tunawaambia wawekezaji jengeni hoteli hapa Mugumu na Tarime ili watu hao wanaokuja kujua kwatu panafananaje wapate pakulala na sisi tunapata pesa, hayo ndiyo mambo tunayotaka kufanya," amesema.
Amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 inaelekeza kuyatazama kwa karibu makundi mbalimbali ya kiuchumi kuboresha shughuli zao ili kuongeza kasi ya maendeleo.
"Ilani yetu inataka tusaidie wakulima, ilani yetu inataka tusaidie wafugaji, tunataka kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.
"Tunataka vijana wachimbaji wa madini wasaidiwe teknolojia ya kuchimba madini ili wapate manufaa. Hayo ndiyo mambo vijana wnatakiwa kuchangamkia," ameeleza.





